Rais Magufuli Aendelea Kupanga Safu Yake, Awateuwa Migiro, Chikawe na Dau

Rais Magufuli Aendelea Kupanga Safu Yake, Awateuwa Migiro, Chikawe na Dau

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ameendelea kufanya uteuzi wake katika maeneo anuai na sasa ameteuwa mabalozi watatu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa. Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa makamishna wanne wa Jeshi la Polisi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, imewataja mabalozi walioteuliwa kuwa ni Dk. Asha-Rose Mtengeti Migiro, Mathias Meinrad Chikawe na Dk. Ramadhan Dau. Vituo vya uwakilishi kwa mabalozi hawa vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia kukamilika.

Kwa upande wa Makamishna wa Polisi, Balozi Sefue amewataja walioteuliwa kuwa ni: Naibu Kamishna wa Polisi Simon Nyakoro Sirro ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi, na ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam. Kamishna Sirro anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Mstaafu Suleiman Kova.

Alisema Naibu Kamishna wa Polisi Albert Nyamuhanga amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Fedha, Utawala na Lojistiki. Kamishna Nyamuhanga anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Clodwing Mathew Mtweve aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.

Mwingine ni Naibu Kamishna wa Polisi Robert Boaz Mikomangwa ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Intelijensia. Kamishna Mikomangwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Valentino Mlowola aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

“..Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Nsato Marijani Mssanzya ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Mafunzo na Operesheni. Kamishna Mssanzya anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Paul Moses Chagonja aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi,” alisema Balozi Ombeni Sefue katika taarifa yake.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amemteua Dk. Modestus Francis Kipilimba kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Kabla ya Uteuzi huu Dk. Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Udhibiti (Director of Risk Management) katika Benki Kuu ya Tanzania. Dk. Kipilimba anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Dikson Maimu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.