Na Mwandishi Maalumu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali itatoa tangazo rasmi la Serikali (Government Notice) kuhusu uanzishaji wa mikoa mipya na wilaya mpya ambalo linatarajiwa kuchapishwa kesho Septemba 9, 2011.
Ametoa kauli hiyo jana jioni Septemba 7, 2011 wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Rukwa na wa wilaya ya Mpanda mara baada ya kuwasili katika kiwanja kidogo cha ndege cha Sitalike katika Hifadhi ya Wanyama ya Katavi na kupokea taarifa ya Mkoa na Wilaya.
“Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alisaini tangazo lile tarehe 5 Septemba, na litatolewa rasmi Ijumaa wiki hii ikiwa ni hatua ya kwanza ya kuonyesha nia ya Mheshimiwa Rais kuanzisha mikoa mipya na wilaya mpya,” alisema.
“Tangazo hili likishatoka litakuwa likionyesha makao makuu ya mikoa mipya na makao makuu ya wilaya yawe wapi. Hivyo wananchi watapata fursa ya kutoa maoni yao kwa muda wa siku 30…wanaruhusiwa kusema kama wanataka mikoa na wilaya vianzishwe au la!”
Alisema wananchi wanapaswa kuzingatia kwamba taarifa zao ni lazima ziwasilishwe makao makuu ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika muda wa siku 30 kuanzia siku ambayo Rais Kikwete alisaini tamko hilo. Waziri Mkuu alisema hatua hiyo inafuatia kukamilika kwa zoezi la kuweka mipaka mipya kutoka kwenye wilaya na mikoa ya zamani na kisha kuchora ramani.
Pinda anatarajiwa kuanza ziara ya siku nne katika mkoa wa Rukwa ambako atazindua matawi mawili ya Chuo Kikuu Huria na tawi la Benki ya CRDB. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Waziri Mkuu anatarajiwa kuzindua tawi la Chuo Kikuu Huria tawi la Sumbawanga Septemba 9, 2011, mjini Sumbawanga.
Septemba 10, 2011, Pinda atakwenda wilayani Mpanda ambako pia atazindua tawi la Chuo Kikuu Huria Mpanda. Mchana huo huo, Waziri Mkuu Pinda atazindua tawi la Benki ya CRDB Mpanda. Hii ni mara ya kwanza kwa wilaya ya Mpanda kuwa na tawi la CRDB. Anatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam Septemba 11, 2011.