Niger haiwezi ‘kumzuia’ Gaddafi kuingia katika nchi hiyo

Waziri wa Mambo ya Nje, Mohamed Bazoum.

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa nchi ya Niger amesema nchi yake haiwezi kufunga mipaka yake kutokea Libya ili kumzuia kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi kukimbilia katika nchi hiyo. Waziri huyo wa Mambo ya Nje, Mohamed Bazoum ameiambia BBC kuwa Gaddafi hakuvuka mpaka wala kuombwa kuvuka mpaka huo.

Alisema hata hivyo msafara wa wanaomtii Gaddafi waliwasili kwenye Mji Mkuu wa Niger, Niamey, na kundi hilo litakuwa huru kubaki au kuendelea na safari. Mamlaka ya mpito ya Libya yamesema yanajaribu kuomba msaada kwa Niger ili kumzuia Kanali Gaddafi kukimbia.

Mkuu wa masuala ya kisiasa Fathi Baja amesema Baraza la Taifa la taifa hilo (NTC) limepeleka ujumbe Niger kujadili “kulinda mipaka yetu kuzuia kupenya kwa aina yeyote ya majeshi ya Kanali Gaddafi Niger, kuzuia jaribio lolote la Gaddafi au familia yake kutorokea Niger”.

Akiulizwa iwapo Niger itafunga mipaka yake, Bw Bazoum alisema: ” Hatuna namna ya kufunga mipaka.Ni mipana sana, na tuna uwezo mdogo sana wa kufanya hivyo.”

Alisema alitumai Kanali Gaddafi hatovuka mipaka, lakini Niger bado haijachukua uamuzi wowote wa aidha kumpokea- au kumkabidhi katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC- iwapo atajaribu kuingia Niger. Mahakama ya ICC inataka kumkamata Kanali Gaddafi, mwanawe Saif al-Islam, na aliyekuwa mkuu wake wa masuala ya kijasusi Abdullah Sanoussi.

Bw Bazoum alisema takriban misafara mitatu ilivuka kutoka Libya kuingia Niger, na hakuna mtoto yeyote wa Kanali Gaddafi aliyekuwemo kwenye misafara hiyo. Maofisa huko Niger walisema mkuu wa usalama wa Kanali Gaddafi, Mansour Daw, ni miongoni mwa walioingia nchini humo siku ya Jumapili. Mke wa Kanali Gaddafi, watoto wake wawili wa kiume na binti yake walikimbilia Algeria wiki iliyopita. Yeye mpaka sasa hajulikani alipo.

NTC inajaribu kufikia makubaliano ya amani katika miji kadhaa ya Libya iliyo na mvutano na inayodhibitiwa na wanaomtii Kanali Gaddafi. Miji hiyo ni pamoja na Bani Walid, Jufra, Sabha na alipozaliwa Kanali Gaddafi mjini Sirte. Baraza hilo la NTC limeweka majeshi nje ya Bani Walid, na kusema mazungumzo yataendelea mpaka siku ya Jumamosi.