Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
SERIKALI kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inategemea kuanza ukarabati wa Miundombinu mibovu hususani ya mitaro inayosababisha maafa wilayani Temeke kuanzia mwezi Mei mwaka huu.
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Ofisa Habari wa Wilaya ya Temeke Joyce Msumba alipokua akizungumza ofisini kwake kuhusu maafa yaliyotokea maeneo ya Sokota, Shule ya Sekondari ya Kibasila na Mtaa wa Butiama ambayo yalisababishwa na ubovu wa miundombinu hiyo.
Hili limetokea baada ya uchunguzi uliofanyika jana ambapo Mhandisi wa Wilaya, Bwana Afya pamoja na Afisa Habari wa Wilaya walifika eneo la tukio na kuona hali halisi.
“Ni kweli maafa hayo yametokea na sababu hasa ni miundo mbinu ya mitaro ambayo ilielekezwa katika maeneo ya makazi ya watu, kwahiyo inapotokea mvua kubwa maji hayaendi yanapostahili na badala yake yanaingia katika nyumba za watu,” alisema Msumba.
Aliongeza kuwa ukarabati huo wa mitaro ni mradi ulio chini ya Dar es salaam Metropolitan Development Project (DMDP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Aidha, Joyce Msumba amesema kuwa endapo mvua kubwa zitanyesha kabla ya mradi kuanza watatumia njia ya kuyanyonya maji kwa pampu na kuyapeleka sehemu husika ili kuzuia maafa yasiendelee kutokea.
Mradi huu unalenga kuhamisha njia za mitaro kutoka kwenye maeneo ya makazi na kuielekeza Bahari ya Hindi ili maji yanayopita katika mitaro hiyo yaende moja kwa moja baharini.