Asilimia 10 tu ya Watanzania Wanamiliki Uchumi-Waziri Mkuu

Waziri Mkuu wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imebuni na kuanza kutekeleza Sera ya Uwekezaji ili kufikia lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi.

“Taarifa zilizopo zinaonyesha ni asilimia 10 tu ya Watanzania ndio wanaomiliki uchumi wa nchi na sera hiyo ndiyo inatoa mwongozo wa jumla unaohakikisha kwamba wananchi wanapata fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo zitawawezesha kujenga na kufaidika na uchumi wa mchi yao,” alisema.

Waziri Mkuu alisema maeneo yanayolengwa na sera hiyo ni yale yenye kuleta matokeo ya haraka na yanayogusa maisha ya wananchi hasa katika sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu, ujenzi, biashara, utalii, madini, viwanda na usafirishaji.

Ametoa kauli hiyo Februari 7, 2016 wakati akizungumza na washiriki wa Mkutano wa Kwanza wa Wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi nchini uliofanyika kwenye ukumbi wa kituo cha kimataifa cha mikutano cha mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inalenga kuhakikisha kuwa sehemu kubwa ya uchumi wa nchi yetu inamilikiwa na Watanzania wenyewe. Waziri Mkuu pia alizindua Mwongozo wa Utekelezaji Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Walemavu, Bibi Jenista Mhagama alisema hadi sasa mikoa 20 imekwishatenga maeneo ya uwekezaji kwenye halamhashauri zake na imeanza kuweka miundombinu ya kuvutia wawekezaji.

Naye Mweyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Prof. Omari Issa alisema katika dunia ya sasa imebainika kuwa haina maana kumpatia mtu mkopo bila kumtafutia masoko au kumuunganisha wadau wa masoko. Kwa hiyo wamejipanga kuwasaidia Watanzania kwa kuwaunganisha na masoko.