Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Serikali imetakiwa kuboresha mazingira bora ya walimu ili kukuza na kuboresha kiwango cha elimu nchini kwani walimu ni kiungo muhimu katika elimu ambacho kinapaswa kupewa kipaumbele kwenye kutimiza azma ya serikali kutoa elimu bora kwa Watanzania.
Mkurugenzi wa Shirika lisilokua la kiserikali la The Foundation for Tommorrow (TFFT) ,Melissa Queyquen ameyasema hayo jana wakati wa utoaji wa tuzo za walimu bora wa shule za msingi za serikali kwa kutambua mchango wa walimu katika maendeleo ya elimu nchini na ustawi bora wa jamii .
Melisa alisema kuwa maendeleo ya taifa lolote lile yanategemea ubora wa elimu waliyonayo watu wake hivyo ni vyema serikali inapofikiria kuboresha elimu ifikirie kuboresha mazingira ya walimu kuanzia kitaaluma wanapoandaliwa kwenda kufundisha ,vifaa vya kufindishia pamoja na stahiki zao.
“Bila Walimu Bora hakuna Elimu Bora ,Tumeamua kuwatia moyo wa walimu kwa kutoa tuzo hizi na vyeti vya kutambua mchango wao ,washindi ni 10 mshindi wa kwanza amepatiwa cheti na shilingi la kitano,na washindi wengine tumewapatia vyeti na fedha taslimu” Alisema Melisa
Afisa Elimu wa Shule za Msingi Wilaya ya Meru Tumsifu Mushi amewataka walimu kufanya kazi ya ualimu kwa moyo na kwa kujituma huku wakitambua kuwa wana wajibu mkubwa wa kuandaa wataalamu watakaoisaidia jamii,taifa na duni jukumu ambalo ni nyeti linapaswa kubebwa kwa uzito unaostahili.
Kwa upande wao walimu waliopewa tuzo hizo Rose Salim wa shule ya Msingi Uraki na Ekaeli Newasha wa Shule ya msingi Kimundo wamesema kuwa kundi la walimu limekua likisahaulika mchango wake katika jamii hivyo tuzo hizo Zimeamsha ari na hamasa ya kufanya kazi kwa bidii.
“Kazi ya ualimu unapaswa uwe unapenda watoto unapenda kuwasaidia waweze kufika mbali kitaaluma ,binafsi nimefanya kazi hii kwa miaka mingi na ninaipenda sana” Alisema Mwalimu Rose Salim