Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya jinai (ICC) imetakiwa kushughulikia malalamiko ya Viongozi wa nchi za Afrika wakiishutumu mahakama hiyo kuwa kandamizi kwa nchi za Kiafrika ile hali makosa ya jinai hutokea karibu kila pembe ya dunia.
Kufuatia shutuma hizo Umoja wa nchi za Afrika (AU) umetoa msimamo wake wa kupinga mahakama hiyo kuonekana kuegemea zaidi kwenye nchi za jangwa la Sahara jambo ambalo linapingwa vikali na viongozi wengi.
Waziri wa Katiba, Sheria na Haki ,Dr.Harisson Mwakyembe akizungumza katika semina iliyoandaliwa na mahakama hiyo ameitaka kufanyia kazi manung`uniko ya bara la Afrika licha ya Tanzania kuunga mkono shughuli za mahakama hiyo lakini bado iko kwenye msimamo wa nchi hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wanasheria Waafrika (PALU) Donald Deya , amesema kuwa mahakama ya ICC inapaswa kujitazama upya na pia viongozi wa Afrika wajitazame pia kwani pande zote mbili zinaonekana kuwa na makosa .
Msajili wa Mahakama ya ICC Herman Von Hebel ameipongeza Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kupigania amani katika nchi jirani hususani Rwanda ambayo ilikumbwa na mauaji ya kimbari na kusisitiza kuwa mahakama hiyo itaendelea kushirikiana vyema na Bara la Afrika katika kutimiza majukumu ya kuleta amani,haki na usawa duniani.
Mahakama ya Kimataifa ya AICC inaendelea na semina ya wiki nzima kwa wanasheria na viongozi mbalimbali juu ya jinsi ya kutumia mahakama hiyo kutetea haki za binadamu na utawala bora.