(Na Raymond Mushumbusi-Dodoma)
Serikali katika kuongeza na kuimarisha uhakika na usalama wa chakula hapa nchini, Serikali imepanga kujenga maghala 275 kwa awamu katika sehemu zenye uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi ambapo hadi sasa jumla ya maghala 125 yanaendelea kujengwa na kukarabatiwa katika maeneo hayo.
Akifafanua hilo wakati akiharisha shughuli za Mkutano wa Pili wa Bunge la 11 lilikuwa na vikao 9 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa,Majaliwa amesema Serikali imejipanga katika kuondoa tatizo la upungufu wa chakula nchini kwa kujenga magala mengi zaidi ya kuhifadhi chakula katika maeneo mbalimbali yenye changamoto za upungufu wa chakula.
. Kassim Majaliwa,Majaliwa amesema hali ya chakula kwa mwaka 2015/2016 katika maeneo mengi ya nchi imeendelea kuwa ya kuridhisha kufuatia mavuno mazuri yaliyopatikana msimu wa kilimo wa 2014/2015 na takwimu za Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinaonesha kuwa albaki kutoka msimu uliopita nchi ilikuwa na ziada ya chakula licha ya kuwepo kwa maeneo machache ambayo hayakuwa na chakula.
“Kutokana na uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2014/2015 kuwa Tani milioni 15.5 na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2015/2016 kuwa Tani milioni 12.9 hivyo nchi imejitosheleza kwa chakula kwa ziada ya Tani milioni 2.5 sawa na asilimia 120 na napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuhudumia maeneo yote yenye uhaba wa chakula”
“Ili kukabiliana na hali ya uhaba wa chakula katika maeneo hayo, Serikali inaendelea kutoa chakula katika maeneo hayo ambapo jumla ya Tani 23,871.6 za chakula zilitengwa kwa ajili hiyo na hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2016, jumla ya Tani 11,860.8 zilikuwa zimechukuliwa toka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwenda kwenye Halmashauri za Wilaya zenye upungufu wa chakula kwa ajili ya usambazaji pia natoa wito kwa Halmashauri ambazo hazijachukua mgao wao kufanya hivyo mara moja ili Wananchi katika maeneo hayo wasizidi kuathirika” Alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha, Mhe Kassim Majaliwa,Majaliwa amesema Serikali kwa kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kujenga maghala ya kimkakati kwa ajili ya kuhifadhi akiba ya Taifa na Kwa sasa ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi Tani 5,000 limeshajengwa Wilayani Mbozi Mkoani Mbeya na Serikali imepata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ambao utawezesha kujenga vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa kuhifadhi Tani 160,000 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 90.
Ameongeza kuwa Pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali, amewataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na watendaji katika Halmashauri zote Nchini kuwahamasisha Wananchi kutumia vizuri mvua zinazonyesha nchini kote kwa kulima kwa bidii ili kuweza kuvuna na kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha kwa ajili ya kaya zao wakati wote wa mwaka na wawahamasishe wafanyabiashara na wadau wengine kusaidia Serikali kuchukua chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka katika maeneo yenye upungufu na kwa kuzingatia maelekezo haya pamoja na juhudi za Serikali zilizooneshwa, tatizo la uhaba wa chakula nchini litapungua, kama siyo kumalizika kabisa.
Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa,Majaliwa amehairisha Mkutano wa Pili Bunge amehairisha shughuli za Bunge mpaka tarehe 19 mwezi April 2016 saa 3 Asubuhi likaporejea katika Mkutano wa kujadili Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017.