Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limewaonya viongozi wa vilabu, wachezaji, waamuzi na wasimamizi wa mchezo kutojihusisha na upangaji wa matokeo (Match fixing) katika michezo inayoendelea sasa katika ligi za ngazi mbalimbali za nchini.
TFF imejipanga na inasimamia vizuri michezo ya Ligi Kuu (VPL), Daraja la Kwanza (FDL), Daraja la Pili (SDL) na Azam Sports Federation Cup (ASFC) inayoendelea na yoyote atakayebainika kujihusisha na mchezo huo wa upangaji matokeo, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa.
Katika michezo yote inayoendelea TFF ina maofisa wake wanaofuatilia kwa ukaribu michezo hiyo, hivyo endapo kiongozi, mchezaji, msimamizi au mwamuzi atabainika kujihusisha na upangaji wa matokeo hatua kali zitachukuliwa .
TFF inawaomba viongozi, wachezaji, wasimamizi wa michezo na waamuzi kutojihusisha na mchezo huo wa upangaji wa matokeo kwani kufanya hivyo ni kukiuka katiba, sheria na kanuni zinaongoza mpira wa miguu nchini.