Na Joachim Mushi
JESHI la Polisi nchini Tanzania, Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya limekamata mzigo mkubwa wa dawa za kulevya ambao unahisiwa ulikuwa usambazwe katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza na vyombo vya habari leo mchana jijini Dar es Salaa, Mkuu wa Kitengo hicho, Geoffrey Nzowa, alisema dawa hizo takribani kilo 97 zinazohisiwa kuwa aina ya Heroine kutoka nchini Pakistan zimekamatwa maeneo ya Barabara ya Bagamoyo na Kunduchi Hoteli.
Alisema watuhumiwa waliokamatwa nazo ni pamoja na Ally Israel raia wa nchini ya Iran, Said Mashaka Mrisho (31) mkazi wa Tandale, Aziz Juma Kizingiti (36) Mkazi wa Magomeni Mapipa, Abdul Lukongo (45) mkazi wa Kariakoo na Hamidu Kitwana (33) mkazi wa Tandale wote wakiwa ni Watanzania kutoka Dar es Salaam. Thamani ya dawa hizo inakadiriwa kufikia kiasi cha sh bilioni tatu fedha za Tanzania.
Ameongeza kuwa mzigo ulikutwa kwenye magari namba T 107 BAS aina ya Carina na namba T 954 BGT aina ya Toyota Carina, watuhumiwa wote wanahojiwa huku uchunguzi ukiendelea na baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani.