Kesi ya Lema yafikia patamu, Jaji ‘awatega’ walalamikaji!

Mbunge wa Arusha Mjini CHADEMA, Godbless Lema

Na Mwandishi Wetu, Arusha

KESI iliyofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na baadhi ya wanachama wa CCM wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Ubunge Jimbo la Arusha Mjini, imefikia hatua ya utata baada ya Jaji Alyoce Mujulizi kuhofia kuibuka kwa suala la vipimo vya vinasaba (DNA).

Jaji Mujulizi ameutega upande wa walalamikaji kuwa endapo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Godbless Lema akiomba mahakamani vifanywe vipimo vya DNA kuthibitisha watoto alionao Dk. Batilda Burian ambaye ndiye aliyeshindwa katika uchaguzi huo huenda vikaleta mzozo mkubwa.

Katika kesi hiyo Musa Nkangaa, Agess Mollel na Happy Kivuyo (ambao ni wanachama wa CCM) wamefungua kesi kupinga matokeo ya Lema, kwamba alitumia maneno ya kumdhalilisha mgombea wa CCM (Dk. Burian) ambayo yaliathiri matokeo ya uchaguzi.

Walalamikaji hao watatu wanadai Lema katika kampeni zake alikuwa akitamka mgombea wa CCM si muaminifu katika ndoa yake na kwamba alikuwa akitoa lugha za kashfa na ubaguzi wa kidini na kijinsia dhidi ya mgombea wao.

Kwa upande wake Jaji Mujulizi alitoa angalizo kwa walalamikaji kuwa njia pekee ya kupata ukweli wa uaminifu wa watoto kwenye ndoa ni kutumia kipimo cha DNA, ambacho kinaweza kuleta mtafaruku na udhalilishaji mwingine bila kujua kutokana na matokeo ya vipimo.

Aidha alisema endapo vipimo hivyo vitadhibitika kama watoto si wa
mume wake wa ndoa inaweza kumletea madhara ndani ya ndoa yake na kama Lema akipinga hajasema maneno hayo, Dk. Burian atakuwa amedhalilishwa kijinsia kama walivyodai walalamikaji.

Jaji Mujulizi alitoa angalizo hilo baada ya kuahirisha kesi hiyo
ambayo itaendelea tena leo na kuwapa nafasi upande wa walalamikaji wajipange na kujadiliana faragha juu ya hilo kabla ya kesi hiyo kuendelea.

“Hoja zilizotolewa na mawakili wa pande zote mbili ni nzito na mambo ni mazito hivyo naomba kesho (leo) asubuhi tukutane faragha kujadili hoja hii ya DNA ili kujua maana suala hili haliwezi kukwepeka.”

Akifafanua zaidi Jaji Mujulizi alisema kikatiba mahakama haiwezi kuamua jambo lolote linalomhusi mtu pasipo muhusika huyo kuwepo mahakamani.

Awali mawakili, Alute Mughwai na Modest Akida waliiomba mahakama kutupilia mbali hoja zilizotolewa na wakili upande wa utetezi Method Kimomogolo dhidi ya mshtakiwa namba moja, Mbunge wa Arusha Mjini, Lema kuwa amemdhalilisha Dk. Burian.

Akimshawishi Jaji Mujulizi, wakili Mughwai alidai madai Lema alitoa lugha za kashfa na ubaguzi wa kidini na kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuongeza kuwa lugha hizo ziliathiri matokeo ya uchaguzi katika jimbo hilo, hali iliyosababisha mgombea huyo wa CCM kushindwa kuchaguliwa.

Naye wakili wa Serikali, Timon Vitalis alidai kuwa kesi hiyo inahusu malalamiko ya udhalilishwaji wa Dk. Burian na si wanachama hao watatu hivyo ni bora ikafutwa kwani kesi hiyo ni maslahi binafsi na si kwa umma.

Hata hivyo wakili upande wa Utetezi, Method Kimomogolo alieleza
mahakamani hapo kuwa hati ya malalalamiko hayo haijajitosheleza na
haijakidhi matakwa ya kisheria hivyo aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali madai hayo kwani mhusika anayetajwa hayupo mahakamani.