Bweni la wanafunzi katika shule ya sekondari ya Edward Lowasa iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha limeteketea kwa moto na wanafunzi zaidi ya 70 wa kidato cha kwanza wamelazimika kupewa likizo ya wiki moja baada ya vitu vyao kuteketezwa na moto ikiwemo magodoro,nguo pamoja na vitabu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Salum Selemani alisema moto huo ambao umetekete za mali zote za wanafunzi na majengo unaodaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme na ulianza saa nne usiku wakati wanafunzi wakiwa darasani wanajisomea na hakuna aliyejeruhiwa japo baadhi yao walikumbwa na hofu iliyosababisha wapoteze fahamu na kukimbizwa hosipitali.
Salum amesema kuwa kwa sasa chanzo cha moto huo kinadaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme ingawa bado uchunguzi zaidi haujafanyika kubaini chanzo cha moto huo licha ya kujiridhisha kuwa wanafunzi wanapokua shuleni hapo hawatumii simu wala chombo chochote cha moto kwa maana ya kiberiti au mshumaa.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya monduli ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Bwana Francis Miti Alisema wanafunzi wote wako salama na wamefikia hatua ya kuwapa likizo fupi ili waweze kutulia wakati jitihada kuwawezesha kuendelea na masomo zikifanyika .
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Monduli Issack Joseph na Mbunge wa jimbo la Monduli Bwana Julius Kalanga alisema kuwa kwa sasa wako kwenye mpango wa kuhakikisha kuwa wanatafuta magodoro na mahitaji muhimu ya kujenga bweni hilo ili wanafunzi waweze kurejea masomoni.
Kalanga amesema kuwa kumekua na matukio ya kujirudia rudia ya shule kuungua moto hivyo walimu ,wazazi na wanafunzi wanapaswa kukaa pamoja na kujadili namna ya kudhibiti matatizo yanayosababisha moto huo pamoja na kuhakikisha kuwa vyombo vya kudhibiti moto (fire extinguisher) vinafungwa kwenye kila jengo la serikali.
Mbunge wa Monduli Julius Kalanga (kulia) akiangalia Bweni la Shule ya Sekondari ya Edward Lowasa lilivyoteketea kwa moto usiku wa kuamkia juzi.Picha, habari na Ferdinand Shayo.
Alisema juhudi za serikali,mashirika na watu binafsi zinahitajika kuhakikisha kuwa bweni jipya linajengwa na wanafunzi wanarejea katika masomo licha ya kuunguliwa na vifaa mbalimbali ikiwemo vitabu,nguo ,magodoro pamoja na masanduku