Kamanda Sabas Akanusha Maandamano ya Madereva Bodaboda Arusha

Kamanda Sabas

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha SACP Liberatus Sabas amekanusha habari iliyoandikwa na gazeti la Jambo Leo la Januari 27, 2016 lenye kichwa cha habari “Waendesha bodaboda Arusha waandamana.

Akiongea kwa njia ya simu Kamanda Sabas alisema hakukuwa na maandamano yoyote ya bodaboda jijini Arusha zaidi ya vijana wachache waendesha bodaboda waliojikusanya kwa Mkuu wa Mkoa.

Kamanda Sabas amesema kuwa, wapo katika operesheni ya waendesha bodaboda ambao wamekuwa wakivunja sheria za barabarani mara kwa mara. Operesheni hiyo ni ya nchi nzima na wameianza Januari 14, 2016.

“Mpaka sasa tumekusanya sh. mil. 21,330,000 ambazo zimetokana na makosa mbalimbali yanayofanywa na waendesha bodaboda wawapo barabarani, makosa hayo ni kutovaa kofia ngumu, kutokuwa na leseni ya udereva, kubeba abiria zaidi ya mmoja, kutokuwa na kadi za pikipiki na kadi za bima,” alisema Kamanda Sabas.

Kamanda Salas amesema kuwa wasingeweza kukusanya kiasi hicho cha pesa kwa kipindi hicho kifupi kama askari polisi wangekuwa wakichukua pesa hizo kwa maslahi yao wenyewe, ila wamekuwa wakiziingiza katika vitabu vya Polisi.

Aidha Kamanda Salas amesema hakuna dereva wa bodaboda anayedaiwa cheti cha udereva bali wametakiwa kuonyesha leseni zao za udereva kwani ndizo zinazothibitisha kwamba wamepitia vyuo vya udereva.

Kamanda Salas amewataka madereva wa bodaboda ambao bado hawajapitia vyuo vya udereva wakajifunze udereva ndipo waendeshe bodaboda na amewaambia kuwa ili wasikamatwe na askari polisi basi wasivunje sheria za barabarani.