Moise Katumbi Chapwe, Rais wa klabu ya TP Mazembe ya DRC amekubali mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ajiunge na KRC Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Samatta anatarajiwa kurejea Dar es Salaam leo kwa ajili ya safari ya Ubelgiji kwenda kuanza maisha mapya katika soka ya Ulaya.
Inafahamika kuwa Samatta tayari amekwisha saini Mkataba wa awali na Genk wa miaka minne na sasa anakwenda kukamilisha taratibu.
Samatta na Genk wanataka kukimbizana na muda ili kuwahi kabla ya dirisha dogo la usajili halijafungwa, angalau mapema Februari Mwanasoka huyo Bora Anayecheza Afrika aanze kucheza Ubelgiji.
Genk wako tayari kutoa Euro 800,000 kumnunua Samatta kutoka Mazembe, ingawa Katumbi alikuwa anataka Euro Milioni 1.
Genk pia imekubali kuipa Mazembe asilimia 20 ya ngawo iwapo itamuuza Samatta klabu nyingine, wakati Katumbi anataka asilimia 25.
Ikumbukwe tayari Samatta amepatiwa viza na Ubalozi wa Ubelgiji kwenda kuanza maisha mapya KRC Genk.