Mgombea Ubunge CCM Igunga arejesha fomu

Mgombea Ubunge Jimbo la Igunga kwa tiketi ya CCM, Dk. Dalaly Peter Kafumu.

NA Bashir Nkoromo, Igunga

MGOMBEA wa Ubunge Jimbo la Igunga kwa tiketi ya CCM, Dk. Dalaly Peter Kafumu amerejesha fomu kwa msimamizi wa uchaguzi na kusema anao uhakika wa kutapata ushindi usio na shaka.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kurejesha fomu hizo ili kuteuliwa rasmi kuwa mgombea, Dk. Kafumu pia ametaja mikakati yake kuwa ni pamoja na kuifanya Igunga kuwa ya kisasa kimaendeleo.

Dk. Kafumu alisema, miongoni mwa atakayoyapa kipaumbele katika kuijenga Igunga ni uboreshaji wa huduma za maji, uboreshaji miundombinu ya barabara hadi vijijini ikiwemo inayounganisha Igunga na Manonga.

Aliahidi kusimamia ujenzi wa daraja la Mbutu kwa kusimamia upatikanaji wa fedha za mradi huo ambazo alisema anafahamu kuwa serikali imeshazitenga na kilichobaki ni usimamizi wa fedha hizo kufika Igunga.

Dk. Kafumu alisema, atasimamia kwa karibu kuhakikisha shule zinapata mahitaji muhimu na pia kusimamia uboreshaji wa kilimo cha pamba na ufugaji ili sekta hiyo ifanyike kisasa zaidi jimboni humi.

“Baadhi ya mambo haya yameshafanywa kwa kiasi chake na mbunge wetu aliyepita Bwana Rostam Aziz, basi nitahakikisha kuanzia pale alipoishia kuyaboresha zaidi na kuanzisha mapya ambayo hataifanya Igunga kupiga hatua ya lkupigiwa mfano hapa nchini”, alisema.

Akijibu swali na Mwandishi wa ITV, Elisante Mkumbo, aliyetaka kujua kama ni hazina gani itakayomwezesha kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo, Dk. Kafumu alisema, ni pamoja na kujulikana kwake kwa wananchi wa jimbo hilo licha ya kuwa ni mzaliwa wa hapo hapo Igunga.

“Najua wakati wa kampeni haujawadia, lakini kwa kuwa mmeniuliza inatosha niwaleleze tu kwa ufupi kwamba nimegombea mara tatu katika kura za maoni za CCM na kila mara nimekuwa nikiwa wa pili hivyo ninaamini wale waliokuwa upande mwingine watakuja sasa
kwangu,” alisema.

Kwa upande wake Msimamizi wa kampeni za CCM jimboni humo, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba alisema wakati Dk. Kafumu ndiye mwenye majawabu ya matatizo ya wananchi wa jimbo hilo tofauti na wa vyama vingine ambao alisema wana majibu tu.

“Unajua kuwa na majibu ni rahisi kuliko kuwa na majawabu, maana majini unaweza kusema ndio au hapana ukawa umejibu hata kama jibu si sahihi, lakini majawabu ni yale ambayo lazima yawe sahihi kwa ajili ya ufumbuzi, hivyo huyu atakuwa nayo majawabu kwa sababu anatumwa na chama ambacho ndicho chenye ilani inayotekelezwa kwa sasa,” alisema Nchemba.

Wakati baadhi ya vyama viliwasindikiza wagombea wao kurejesha fomu kwa sherehe, CCM walirejesha kwa utulivu kwa heshima ya mtoto aliyefariki dinia kwa kugongwa na lori akiwa katika kundi la wananchi waliokuwa wakisubiri msafara wa mgombea wa ubunge wa CCM.

“Kama mnavyoona leo pia tumefanya kama wakati wa kuchukua fomu, hatukufanya shamra shamra, sio kwamba hatuwezi la, imebidi tifanye hivi kwa kuwa majozi ya kifo cha yule mtoto bado yametanda, badala yake tunawaomba wana-CCM na wale mashabiki wote kujitokeza kwa wingi siku ya uzinduzi wa kampeni zetu ambao utafanyika Jumamosi kwenye viwanja vya Sokoine hapa mjini,” alisema Mwigulu.

Baada ya CCM wagombea wa vyama vya DP na vyama vingine kikiwemo CHADEMA na CUF waliendelea kurejesha fomu na hadi kwa ajili ya kutoa nafasi kwa Msimamizi wa uchaguzi kuzipitia fomu zao na kuwatangaza rasmi wagombea waliopita. Uchaguzi mdogo jimbo la Igunga umepangwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu kufuatia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Rostam Aziz kujiuzulu kutokana na sababu za kisiasa, na kampeni zinaanza kutimua vumbi leo.