Mambo Yaharibika NIDA, Rais Amsimamisha Mkurugenzi

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiongea na waandishi wa habari (hawapo) leo jijini Dar es salaam kuhusu uamuzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya kiasi cha Sh. Bilioni 179.6 zilizotumika hadi sasa. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu Gerson Msigwa.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiongea na waandishi wa habari (hawapo) leo jijini Dar es salaam kuhusu uamuzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya kiasi cha Sh. Bilioni 179.6 zilizotumika hadi sasa. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu Gerson Msigwa.

Na Eleuteri Mangi-MAELEZO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bw. Dickson Maimu na kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya kiasi cha Sh. Bilioni 179.6 zilizotumika hadi sasa.

Uamuzi huo wa Rais wa kutengua na kusimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu huyo umetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es salaam. Sambamba na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu NIDA, Rais Dk. Magufuli pia amewasimamisha kazi watendaji wanne wa Mamlaka hiyo ambao ni Mkurugenzi wa TEHAMA Joseph Mkani, Afisa Ugavi Mkuu Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria Sabrina Nyoni na Afisa Usafirishaji George Ntalima.

Balozi Sefue alisema kuwa Rais ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wamanunuzi yote yaliyofanywa na NIDA, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA ikiwemo “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) kujiridhisha na kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.

Aidha, Rais Dk. Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne Mahadhi Juma Maalim kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait kufuatia uamuzi wa Serikali kufungua Ofisi ya Ubalozi katika nchi hiyo rafiki.

Vile vile Rais ameagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi wawili ambao mikataba yao imeisha na kuwataka Mabalozi hao kukabidhi kazi kwa Afisa Mkuu au Mwandamizi aliyechini yao leo hii.

Mabalozi hao ni Bi Batilda Salha Buriani, aliyeko Tokyo, Japan, Dk. James Alex Msekela, aliyeko Rome, Italia. Kwa mujibu wa Balozi Sefue, Rais pia amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Bwana Peter Allan Kallaghe ambaye anarejea Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa ambapo atakapopangiwa kazi nyingine.

Balozi Sefue alisema kuwa hadi sasa vituo vya Ubalozi ambavyo viko wazi ni London nchini Uingereza kufuatia kurejea nchini kwa Balozi Peter A. Kallaghe, Brussels nchini Ubelgiji kufuatia aliyekuwa Balozi, Dk. Deodorous Kamala kuchaguliwa kuwa Mbunge, Rome nchini Italia, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Dk. James Alex Msekela na Tokyo nchini Japan, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Bibi Batilda Buriani.

Vituo vingine vya Ubalozi ambavyo viko wazi ni Kuala Lumpar nchini Malaysia, kufuatia aliyekuwa Balozi Dk. Aziz Ponray Mlima kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa na Brasilia nchini Brazil, kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Balozi, Francis Malambugi.

Wakati huo Balozi Sefue alisema kuwa Rais ametengua uteuzi wa Mhandisi Madeni Juma Kipande kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.