Mashindano ya kuwania kombe la Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani CHAN yaliendelea kutifua vumbi nchini Rwanda, wenyeji wakichapwa 4-1 na Morocco jana Jumapili.
Ivory Coast nao waliinyuka Gabon kwa kichapo sawa, zikiwa ni mechi za mwisho za kundi A. Wenyeji Rwanda, timu ya Amavubi walichapwa vikali goli 4-1 katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa taifa Amahoro.
Dakika 44 tu za kipindi cha kwanza zimetosha kuihakikishia ushindi Morocco iliyocheza mchezo mzuri dhidi ya wenyeji ambao kocha Mc Kinsley aliamua kuwapumzisha wachezaji 8 wa kikosi cha kwanza.
Mabao ya Morocco yalifungwa na Abdelghani Mouaoui (mawili), Mohamed Aziz na Abdeladim Khadrouf. Hegman Ngomirakiza alifungia wenyeji bao la kufutia machozi.
Mechi za kundi A zilichezwa kwa wakati mmoja, ila viwanja tofauti. Katika uwanja wa Huye, kusini mwa Rwanda, Ivory Coast waliisambaratisha Gabon kwa kuinyuka 4-1. Mabao ya Ivory Coast yalifungwa na Aka Essis, Djedje Guiza, Koffi Boua na Nilmar Ble. La gabon lilifungwa na Franck Obambou.
Timu zote mbili Rwanda na Ivory Coast zimemaliza michuano ya makundi zikiwa na alama 6 lakini Rwanda inashika usukani kwa kuwa matokeo ya mechi iliyowakutanisha Rwanda ilipata ushindi wa 1-0.
Leo Jumatatu zitachezwa mechi za mwisho katika kundi la pili ambapo kwenye uwanja wa Huye, Cameroon itapambana na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wakati huo huo kwenye uwanja wa taifa Amahoro Ethiopia itamenyana na Angola.
DR Congo tayari ina alama 6 na Cameroon ina alama 4, ikiwa na maana kuwa mshindi wa mechi hii ndiye atakayeongoza kundi hili. Pia Ethiopia ina nafasi japo finyu sana.
Ikiwa Cameroon itapoteza dhidi ya Congo na Ethiopia kuifunga Angola, itahesabiwa akiba ya magoli baina ya Cameroon na Ethiopia.