Wafanyakazi wa Mizani Watakiwa Kuonesha Uwazi, Uadilifu na Weledi

Mkuu wa Mizani Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Lucian Kilewo akifafanua jambo katika mafunzo ya kuwajengea uelewa wa pamoja maafisa uendeshaji wa Mizani yanayofanyika mjini Morogoro. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa matengenezo wa TANROARDS Eng. Joseph Lwiza akifuatiwa na Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Julius Chambo na Kaimu Mkurugenzi msaidizi Eng. Joyce Mbunju.

Mkuu wa Mizani Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Lucian Kilewo akifafanua jambo katika mafunzo ya kuwajengea uelewa wa pamoja maafisa uendeshaji wa Mizani yanayofanyika mjini Morogoro. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa matengenezo wa TANROARDS Eng. Joseph Lwiza akifuatiwa na Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Julius Chambo na Kaimu Mkurugenzi msaidizi Eng. Joyce Mbunju.

WAFANYAKAZI wa Mizani hapa nchini wametakiwa kufanya kazi kwa uwazi, uadilifu, na weledi ili kuzingatia sheria zinazoongoza sekta hiyo na hivyo kutenda haki kwa wasafirishaji wote na kujenga taswira nzuri kwa taasisi hiyo. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Julias Chambo katika mafunzo kwa maofisa waendesha mizani hapa nchini yanayofanyika mjini Morogoro.

“Sasa tubadilike tujenge taswira njema katika sekta ya mizani kwa kuepuka vitendo vya rushwa kwa kufanya kazi kwa uwazi na kulinda barabara zetu,” amesema Eng. Chambo.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uelewa wa pamoja watumishi wote wa mizani nchini juu ya utelekelezaji wa majukumu yao na kupunguza malalamiko yasio na msingi katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.

Naye mkuu wa mizani wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng Lucian Kilewo amewataka watumishi wa mizani kutumia elimu walioipata katika kutekeleza majukumu yao na kuipeleka kwa wenzao ili sekta hiyo ipate mabadiliko yanayoendana na wakati wa sasa.

“Mafunzo haya yataendelea mara kwa mara ili kuhakikisha mnakuwa na uelewa wa pamoja katika kuimarisha sekta ya mizani nchini na kuiwezesha kufanyakazi kwa tija na kulinda barabara zinazojengwa kwa fedha nyingi,” amefafanua Eng. Kilewo.

Mkurugenzi wa matengenezo (TANROADS) Eng. Joseph Lwiza amesema Wakala wa Barabara nchini wamejipanga kutatua changamoto zinazojitokeza katika vituo vya mizani nchini kote na kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha kazi zinazofanywa katika mizani kuonekana moja kwa moja makao makuu ya TANROADS na Wizarani ili kuimarisha uwazi na kudhibiti rushwa.

Wataalam hao wa mizani pia wametembelea mizani zinanopima uzito wa magari katika mwendo weigh in motion katika eneo la Mikese na Vigwaza na kujionea mfumo huo unavyofanya kazi na kupunguza msongamano wa magari. Takriban mizani 70 zinapima uzito wa magari hapa nchini tatu zikiwa za magari yanayopimwa yakiwa katika mwendo, 29 mizani za kuhamisha-mobile na 41 mizani za kudumu –fixed ambapo nia yake ni kuhakikisha magari yababeba uzito unaokubalika ili kulinda barabara.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.