Samatta Atua TP Mazembe Kutoa Mkono Wa Kwaheri

Samatta

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta alitarajia kuondoka asubuhi ya jana kwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kujiunga na klabu yake, TP Mazembe wakati sakata la uhamisho wake likiendelea.

Samatta anaondoka na Maofisa wa Wizara ya Michezo walioteuliwa kwenda kuzungumza na Rais wa TP Mazembe, Moise Katumbi kumshawishi amruhusu mchezaji huyo kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji.
Lakini iwapo Katumbi ataendelea kusistiza msimamo wake wa kutaka Samatta aende Nantes ya Ufaransa, basi mchezaji huyo ataamua kubaki Mazembe amalizie miezi yake mitatu ya Mkataba wake ili aondoke kama mchezaji huru Aprili.

Genk wako tayari kutoa Euro 800,000 kumnunua Samatta kutoka Mazembe, lakini Moise amesema anataka Euro Milioni 1. Aidha, Katumbi anataka asilimia 25 ya mgawo iwapo klabu itakayomnunua Samatta itamuuza kwa klabu nyingine.

mbwanasamata

Moise anasema Nantes wamekubali kutoa Euro Milioni 1 na mgawo wa asilimia 25, wakati Genk wamekomea kwenye Euro 800,000 na ofa ya mgawo ya asilimia 20 mchezaji huyo akiuzwa klabu nyingine.

Genk inaona miezi mitatu aliyobakiza Samatta Mazembe ni michache kutoa zaidi ya Euro 800,000 kumnunua na mgawo wa zaidi ya asilimia 20 iwapo itamuuza sehemu nyingine na hapo ndipo wanapotofautiana na Katumbi.

Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo anaamini kwa msimamo wa Samatta kutaka amalizie Mkataba wake Mazembe ili aondoke kama mchezaji huru Aprili, Katumbi anaweza kulainika na kumruhusu nyota huyo aliyeibukia Mbagala, Dar es Salaam ili asikose kabisa.

Na Genk ambao tayari wamekwishasaini Mkataba wa awali na Samatta wapo tayari kumsubiri hadi Aprili atakapomaliza Mkataba wake ili aanze kucheza Agosti.