Rwanda imekuwa timu ya kwanza kufuzu kwa robofainali ya michuano ya taifa bingwa Afrika kwa wachezaji wa ndani baada ya kuilaza Gabon.
Rwanda, ambao ni wenyeji, wameandikisha ushindi wa 2-1 dhidi ya Gabon, kwenye mechi hiyo iliyochezewa uwanja wa Amahoro.
Mabao ya Rwanda yamefungwa na Sugira Ernest,Bao la kwanza mwishoni mwa kipindi cha kwanza na la pili likifungwa mapema kipindi cha pili.
Rwanda ilifungua michuano hii kwa kucharaza Ivory Coast bao 1-0, ambao nao wameifunga Morocco katika mchezo wa pili bao 1 -0.
Nao Mali walitoka nyuma mara mbili na kulazimisha sare ya 2-2 mechi ya taifa bingwa Afrika kwa wachezaji wa ndani kati yao na Uganda.
Mechi hiyo ilichezewa mjini Rubavu, Rwanda. Kwenye mechi nyingine ya Kundi D, Zambia waliwanyuka majirani zao Zimbabwe 1-0.
Nahodha wa Uganda Farouk Miya alisaidia kufunga bao la kwanza na kisha akawafungia bao la pili kabla ya kuondolewa wakati wa mapumziko baada ya kuumia.
Bao la kwanza la Uganda lilifungwa kwa kichwa na Joseph Ochaya kipindi cha kwanza. Mali walisawazisha dakika 12 baadaye kupitia Sekou Koita.
Dakika nne kabla ya mapumziko, Miya aliwafungia Uganda bao la pili kupitia mkwaju wa penalti baada ya Erisa Ssekisambu kuchezewa visivyo.
Uganda chini ya kocha Milutin ‘Micho’ Sredojevic hata hivyo walipata pigo Miya alipoumia na kushindwa kurejea kwa kipindi cha pili.
Kipa wao Watenga pia aliumia na msaidizi wake Mathias Kigonya akaingia nafasi yake.
Mali walisawazisha kupitia mshambuliaji Hamidou Sinayoko baada yake kupata pasi kutoka kwa Mamadou Coulibaly.
Mechi zijazo katika Kundi zitachezwa Jumamosi, Zimbabwe dhidi ya Mali nao Uganda wakabili Zambia.