Wananchi Watakiwa Kujitokeza Kuliombea Taifa

Mwenyekiti wa Good News for All Ministry, Askofu Charles Gadi

Mwenyekiti wa Good News for All Ministry, Askofu Charles Gadi

Na Beatrice Lyimo- Maelezo

Mwenyekiti wa Good News for All Ministry, Askofu Charles Gadi ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kumuomba Mungu dhidi ya hali ya hewa ya joto kali nchini.

Askofu huyo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar e s Salaam mara baada ya Mamlaka ya hali ya hewa kuonyesha hali ya joto kufika nyuzi joto 35°C.

Askofu Gadi ameongeza kuwa, wanatarajia kufanya mkutano wa maombi siku ya Jumatano ya tarehe 20 Januari mwaka huu katika eneo la Soko la Samaki maarufu kama Feri ili kuomba Mungu kuepusha ongezeko la joto nchini.

“Joto limesambaa katika maeneo ya pwani hususani Dar es Salaam, Tanga, na visiwa vya Zanzibar, hivyo kwa hali hii tumeona tufanye mkutano wa maombi mafupi katika eneo la Soko la samaki la feri siku ya Jumatano kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana,

“Mungu amenipa nafasi ya kuomba dhidi ya majanga ya kimazingira kama haya hivyo tunawakaribisha watu wote wa Dar es Salaam tuje tumlilie Mungu kwa pamoja ili tuondokane na janga hili la joto na madhara ya Elnino” alifafanua Askofu Gadi.

Kwa upande wake katibu wa Good News For All Ministry Mchungaji Palemo Massawe amewataka Wananchi kuchukua hatua ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kufanya usafi katika mazingira yanayowazunguka.

Uongozi huo unaendelea na maombi ya kumuombea Rais John Pombe Magufuli kufanikiwa katika juhudi zake za kulikomboa nchi kiuchumi na kielimu.