Yanga Sc Yajikita Kileleni Ligi Kuu Tanzania Bara

Yondani-6

Yanga SC imerejea kileleni mwa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara baada ya ushindi mwembamba walioupata jana Jumapili January 17, 2016 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara kwenye mchezo ambao umechezwa kwenye uwanja wa taifa, Dar es Salaam.

Haikuwa kazi rahisi Yanga kuibuka na ushindi mbele ya Ndanda kwani dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika huku timu hizo zikiwa hazijafungana. Kipindi cha pili Yanga walirudi na kuanza kulazimisha ushindi kufuatia kukaziwa katika kipindi cha kwanza kitu ambacho kilizaa matunda kwa upande wao baada ya kufanikiwa kupachika bao pekee ambalo limewapeleka kileleni mwa VPL.

Goli la Yanga limefungwa na Kelvin Yondani dakika ya 60 kipindi cha pili kwa mkwaju wa penati baada ya Deus Kaseke kuangushwa na beki wa Ndanda kwenye eneo la hatari.

Yondani-5

Hiyo ilikuwa ni penati ya pili kwa upande wa Yanga kwenye mchezo wa leo, penati ya kwanza iliyopigwa na Amis Tambwe iligonga ‘mtambaa panya’ na kurudi uwanjani ambayo ilitokana na Simon Msuva kuangushwa ndani ya 18 na Ndanda FC.

Ushindi wa Yanga dhidi ya Ndanda unawafanya wafikishe pointi 36 sawa na Azam FC na kufanikiwa kurejea kileleni mwa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara kufuatia sare ya juzi waliyoipata Azam dhidi ya African Sports ya Tanga.

Yanga inaongoza ligi kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, Azam wanabaki nafasi ya pili huku nafasi ya tatu ikikamatiwa na Simba iliyofikisha pointi 30 baada ya kuifunga Mtibwa kwenye mchezo wa jana, Mtibwa Sugar inahika nafasi ya nne kwa pointi 27 na nafasi ya tano ipo Stand United ikiwa na pointi 25.

Msimamo-vpl