Filamu ya Revenant imepata tuzo katika hafla ya mwaka huu ya Golden Globes baada ya kushinda taji kuu la filamu yenye mchezo bora wa kuigiza.
Nyota wa filamu hiyo Leonardo Di Caprio alishinda tuzo la mwigizaji bora huku Alejandro G Inarritu akishinda kwa ulekezaji bora.
Filamu ya Ridley Scott,The Martian ilishinda tuzo la filamu bora ya vichekesho ikiwa ni tuzo jengine la Matt Damon
Nyota wa Filamu ya Room Star ,Brie Larson alitajwa kuwa mwigizaji bora upande wa wanawake huku Jennifer Lawrence akishinda taji la mwigizaji bora wa filamu ya vichekesho upande wa wanawake.
Miongoni mwa raia wa Uingereza walioshinda ni pamoja na Kate Winslet, aliyetuzwa taji la msaidizi bora upande wa wanawake katika uigizaji wa filamu ya Steve Jobs,huku mwanamuziki Sam Smith akishinda tuzo kwa wimbo wake Writing on the Wall.
Nyota wa filamu maarufu kwa jina Sylvester Stallone alijishindia tuzo la nyota bora msaidizi kwa filamu yake ya Rocky Balboa in Creed.
Na kama ilivyotabiriwa filamu ya Pixars inside out ilishinda tuzo la filamu bora ya vibonzo huku mtunzi wake raia wa Itali Ennio Morricone akishinda tuzo la tatu la Golden Globe kwa filamu ya Quentin Tarantino,The Hateful Eight.
Filamu ya Amazon ilishinda tuzo kuu zaidi katika kitengo cha televisheni huku ikishinda mataji mawili kwa vipindi vya Original Drama,Mr. Robot na Mozart in the jungle.
Nyota wa filamu za Mexico Gael Garcia Bernal alishinda tuzo la mwigizaji bora katika filamu ya vichekesho kwa uigizaji wake katika Mozart in the Jungle huku Christian Slater akishinda tuzo ya mwigizaji msaidizi katika kipindi cha msururu cha Mr.Robot.
Baada ya kushinda taji la Emmy mnamo mwezi Septemba ,nyota wa filamu ya Empire Taraji P Henson alishinda tuzo ya mwigizaji bora upande wa wanawake katika kipindi cha msurusu cha Televisheni huku Nyota wa kipindi cha Mad Men Jon Ham akishinda tuzo lake la pili la Golden Globe kwa kuwa mwigizaji bora,miaka minane baada ya kushinda tuzo yake ya kwanza wakati filamu hiyo ilipoanza.
Lakini usiku wa hafla hiyo ulitawaliwa na filamu ya Alejandro G Inarittu,The Revenant iliomarika kupitia uwelekezaji wa Inarritu na uwigizaji wa DiCaprio.
Filamu hiyo pia imemuweka DiCaprio katika kilele cha uwigizaji baada ya kushindwa kushinda tuzo yoyote katika kipindi kirefu cha uwigizaji wake