RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amempongeza Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Ali Samatta kwa kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani Afrika kwa mwaka 2016.
Pongezi hizo amezitoa leo Jijini Dar es salaam alipokuta na Naodha huyo katika Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizopo Lumumba Jijini Dar es salaam. Dk. Kikwete alimpongeza Nahodha huyo (Mbwana Samatta) na kumtaka kuongeza juhudi zaidi ili aweze kucheza katka Ligi kubwa Barani Ulaya.
“Natamani siku moja tuwe tunakuangalia Samatta ukifunga magoli katika Ligi kubwa Barani Ulaya kama vile Ligi kuu ya Uingereza” Alisema Dkt Kikwete. Kwa upande wake, Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye alisema kuwa Wizara imepata faraja kubwa kwa Samatta kuiwakilisha Tanzania katika tuzo hizo za Kimataifa kwa kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro hicho.
Aidha, Mbwana Samatta alisema kuwa, anamshukuru Rais mstaafu Mhe. Dkt. Kikwete kwa kumpa moyo wa kupambana na ameishukuru pia Serikali ya Awamu ya tano kwa kumuunga mkono katika kupeperusha bendera ya taifa katika soka la kimataifa.
Samatta aliibuka kuwa Mchezaji Bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya Afrika baada ya kuwabwaga wenzake wawili kwenye kinyang’anyiro hicho, akiwemo mchezaji mwenzake wa TP Mazembe,Kipa Robert Kidiaba pamoja na Mualgeria,Baghdad Boundjah anayeichezea Klabu ya Etoile Du Sahel ya nchini Algeria.