Mbwana Samatta ndio jina liliotajwa zaidi kwenye vinywa vya watanzania wengi na Afrika kiujumla ndani ya masaa kadhaa yaliyopita baada ya mwanasoka huyo wa Kitanzania anayekipiga katika klabu ya TP Mazembe kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika Anayecheza Ligi za Ndani ya Afrika.
Mbwana Samatta alipata jumla ya kura 127 na hivyo kuongoza, akifuatiwa kwa mbali na mchezaji mwenzie wa TP Mazembe Robert Kidiaba aliyepata kura 88 na aliyefunga Top 3 ni Baghdad Bournedjah. Kura zilipigwa na mataifa 45 ya nchi wanachama wa shirikisho la soka Afrika CAF.
Ushindi wa Samatta, ambaye ni mshindi wa na mfungaji bora wa ligi ya mabingwa wa Afrika umetokana na kuwashinda wapinzani wake Zein Edin Farahat, Roger Assale, Robert Kidiaba, Moudather el Tahir,Mohammed Meftah, Kermit Erasmus, Felipe Ovono, Baghdad Bournedjah, na Abdeladim Khadrouf.
Utaratibu wa CAF – Shirikisho la soka katika upigaji kura wa kumchagua mshindi wa tuzo hii unatokana na kura zilizopigwa na makocha wa timu za taifa au wakurugenzi wa ufundi wa vyama vya soka vya nchi za kiafrika.
Naye Thomas Ulimwengu amejikuta akishindwa kutoa neno kwa pacha wake Mbwana Samatta, kutokana na furaha aliyokuwa nayo baada ya Samatta kunyakua tuzo ya mchezaji bora Afrika 2015 kwenye tuzo za Glo-Caf Awards zilizofanyika usiku wa January 7, 2016 Abuja, Nigeria.
Samatta na Ulimengu wamecheza kwa pamoja na kwa mafanikio makubwa sana kwenye klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ulimwengu ame-post kwenye account yake ya twitter ujumbe unaoashiria furaha yake kufuatia Samatta kutwaa tuzo hiyo.
Ujumbe wa Thomas Ulimwengu ulisomeka: “Nashindwa kuonyesha hisia zangu, kwa tuzo kubwa kama hii uloipata pacha..Hongera sana @samagoals Mungu ametimiza maombi yetu..”, hayo ni maneno yaliyoandikwa kwenye account ya twitter ya Thomas Ulimwengu.