Na Nyakongo Manyama na Scolastika Tweneshe-MAELEZO
MKOA wa Mwanza unatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kumwombea Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na Taifa kwa ujumla. Maombi hayo yanatarajiwa kufanyika Jumatano ya wiki ijayo katika Viwanja vya Furahisha.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Good News For All Ministry Askofu Dk. Charles Gadi wakati wa mkutano wake na waandishi wa wahabari jijini Dar es Salaam. Amesema kuwa wanachukua fursa hiyo kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasaidizi wake kwa kutambua kazi nzuri anayoifanya ya kupambana na ufisadi na kuleta maendeleo ya nchi na watu wake.
Askofu huyo ameongeza kuwa sanjari na maombi ya kuwaombea viongozi, pia wataiombea Tanzania ili iepukane na majanga mbalimbali kama vile ukame, njaa na mvua za el-nino ambayo yanaweza kusababisha maafa kwa wananchi. Ameongeza kuwa katika maombi hayo mkutano utapata fursa ya kutubu na kumwomba Mungu alete mvua za kusaidia wananchi na wanyama wa kufugwa na wa mwituni.
“Tutamwomba Mungu ili nchi yetu ijitosheleze kwa chakula na pia iweze kuuza akiba nje na kutuletea fedha za kigeni,” alisema Askofu Dk. Gadi.