KAMPUNI ya Simu nchini Tanzania (TTCL) imeamua kusherehekea Siku Kuu ya Mwaka Mpya 2016 pamoja vituo vya watu wenye mahitaji maalum, wanaoishi katika mazingira magumu na wazee wasiojiweza kwa kutoa msaada wa vyakula, vinywaji na mavazi kwenye vituo vitatu tofauti jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana wakati wa zoezi la kutembelea vituo hivyo na kukabidhi msaada kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura, Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Nicodemas Thomas Mushi alisema wameamua kusherehekea siku kuu ya mwaka mpya kwa kutoa chakula na vinywaji kwa baadhi ya vituo hivyo ili kuungana na familia hizo hasa kipindi hiki cha siku kuu ili kuwapa faraja na matumaini watu hao wenye uhitaji.
Alisema vyakula vilivyotolewa ni pamoja na mifuko ya mchele, unga, sukari, maharage, mafuta ya kupikia na maji safi ya kunywa. Msaada huo pia unajumuisha fulana zenye nembo ya Ttcl ambavyo vyote vina thamani ya shilingi milioni nne fedha za Kitanzania, ambapo vyote wameomba vitumike katika kipindi hiki cha siku kuu ya mwaka mpya.
Meneja huyo wa Uhusiano wa TTCL alivitaja vituo vilivyonufaika na msaada huo ni pamoja na Kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Kiwohede kilichopo Buguruni Malapa, Kituo cha Kulelea Watoto Wanaoishi katika Mazingira Magumu cha Honoratha cha Temeke na Kituo cha Makazi ya Wazee cha Nunge kilichopo Kigamboni vyote vya jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa ni kawaida ya kampuni hiyo kuungana na jamii hasa makundi ya waitaji kila inapokuwa na fursa ikiwa ni utaratibu waliojiwekea kurejesha sehemu ya mapato yao kwa jamii ambao ndio wateja wa kampuni hiyo. “…Hii sio mara ya kwanza kwa TTCL kuungana na familia kama hizi kwa kutoa chochote ikiwa ni kutambua mchango wao katika taasisi yetu, tutaendelea kufanya hivi kila inapopatikana fursa ndani ya kampuni yetu,” alisema Mushi.
“…Mwaka 2015 umekuwa na mafanikio makubwa kwetu, tumewahudumia Wananchi, wateja wetu na wadau wote kwa ufanisi mkubwa. Tumeweza pia kuingiza bidhaa mpya sokoni, mtandao wa Intaneti wenye kasi kubwa wa 4G LTE.. Tunawaomba Watanzania na wateja wetu wote watuunge mkono zaidi mwaka 2016 ambapo tutaboresha zaidi huduma zetu..,” alisema Thomas.
Kwa upande wake Mlezi wa Watoto na Vijana, Stella Mwambenja wa Kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Kiwohede kilichopo Buguruni Malapa akipokea msaada huo kwa kituo chao aliishukuru kampuni ya TTCL kwa kuikumbuka jamii ya wasiojiweza hasa kipindi hiki cha siku kuu ambapo familia hizo uhitaji faraja zaidi.
Naye Ofisa Mfawidhi wa Kituo cha Makazi ya Wazee Nunge kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, Ojuku Mgezi akipokea msaada huo katika kituo chake aliyaomba makampuni mengine na jamii kwa ujumla kuiga mfano wa kampuni ya TTCL kwa kuvikumbuka vituo ambavyo huitaji zaidi msaada wa jamii. Alisema jukumu la msaada wa vituo kama hivyo havipaswi kubebwa na Serikali pekee bali jamii yote ikiwa ni pamoja na kuangalia mbinu mbadala la kutatua changamoto ndani za vituo hivyo.