Wanakijiji Enguserosambu Wafurahia Msitu Kurejeshwa Mikononi mwao

Watendaji wa PALISEP wakiwa pamoja na wanajamii wakishikana mikono kuonesha ushirikiano baina yao. Kuanzia kushoto ni Sarah Saningo, Robert Kamakia, Jackson Nangiria, Norkiyengop Mbaima, Sunde Tutayo na Fredy Samberu

Watendaji
wa PALISEP wakiwa pamoja na wanajamii wakishikana mikono kuonesha
ushirikiano baina yao. Kuanzia kushoto ni Sarah Saningo, Robert Kamakia,
Jackson Nangiria, Norkiyengop Mbaima, Sunde Tutayo na Fredy Samberu

Mraghbishi Noorkiyengop Mbaima toka kijiji cha Enguserosambu akisimama mbele ya mifugo iliyokutwa
msituni  katika eneo lililoruhusiwa la msitu wa  jamii wa Enguserosambu

Ilikuwa ni siku ya shangwe na furaha kwa wananchi wa kata ya Enguserosambu wilayani Ngorongoro. Hii ni baada ya serikali kukubali ombi lao la kusimamia rasilimali  ya msitu wa Loliondo namba 2 unaopakana na vijiji vinne vinavyokadiriwa kuwa na idadi ya wakazi wapatao 20,000 wanaotegemea mahitaji yao toka katika huo msitu.
Huu ni msitu pekee ambao wananchi kwa kushirikiana na Mkuu wao wa wilaya, na mashirika rafiki, wamefanikiwa kuishawishi serikali kuukabidhi msitu huo kwao.  Katika mchakato huo uliochukua miaka kadhaa wanawake toka katika vijiji vya Enguserosambu, Ng’arua, Orkiu na Naan  wamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha azma hiyo ya kubakiza msitu wao wa enzi mikononi mwao.
Akielezea furaha yake aliposikia msitu wa Loliondo namba 2 umekabidhiwa kwa wananchi, mraghbishi mwanamke Noorkiyengop Mbaima alisema
“Mimi mwenyewe nimefurahia, kwa sababu sisi akina mama tunategemea sana msitu huu kwa mahitaji yetu. Huu msitu kama ungeondoka katika mikono ya jamii basi tungeathirika sana sisi kina mama.” Umuhimu wa msitu huu kwa kina  mama ndio uliowapelekea wao kutunga na kuimba nyimbo za hamasa na kutumbuiza, kushiriki kwa wingi katika vikao mbalimbali vya maamuzi wakati wote wa mchakato huo. Kwa kuwa msitu huu ndio tegemeo lao katika kuendesha maisha ya kila siku. Hakuna chochote ambacho kiliamriwa bila ya wao kuchangia na kushirikishwa kuanzia utungaji wa sheria ndogongogo za usimamizi wa msitu hadi kukabidhiwa rasmi msitu huo. “Nikichukulia mfano katika mikutano yote ya vijiji. Kiukweli wanawake wamekuwa wanajitokeza
kwa wingi, kuliko makundi mengine yoyote. Hata ile siku ya uzinduzi wa msitu walikuwa wengi zaidi,” anaelezea Jackson Nangiria

Ushiriki huu wa wanawake unatokana na ukweli kwamba wanauhusiano wa karibu na msitu huo wa enzi wa Enguserosambu.Si kwa ajili yao tu pamoja na watoto wao pia. Ni watoto hawa wa kike wenye majukumu ya kujenga nyumba kwa kutumia miti inayotoka ndani ya msitu huu, ndio wanaotembea na punda wakiwabebesha maguduria ya maji kwa umbali mrefu wakitafuta maji ambayo chanzo chake kipo kwenye  msitu huu. Wanapopata watoto wanahitaji dawa za kuwaogeshea na dawa za uzazi ambazo zinatoka kwenye msitu huu. Wao ndio wapishi katika familia zao hivyo wanahitaji kuni zinatokana na miti iliyoanguka na kukauka ambayo inapatikana kwenye msitu huu.  “Kina mama wanafanya mitambiko ndani ya msitu huu wengine ambao hawakupata watoto wanapatia hapo baada ya kuomba ndani ya msitu huu. Si hivyo tu ndani ya msitu huu kuna dawa mbalimbali za asili kwa mfano mtoto akizaliwadawa ya kumwogesha na kumnawisha hupatikana humo humo na nyingine ni za kunywa kama maziwa na nyingine kwa ajili ya mama,” anaeleza mwanamama mraghbishi Noorkiyengop Mbaima.   Uwepo wa wanawake hawa wa Kimasai katika kata ya Enguserosambu kiukweli unatokana na uwepo wa msitu huu.  Huu ndio msitu wa enzi ambao serikali ilipendekeza uwe chini ya usimamizi wake kama ulivyokuwa msitnamba moja wa Loliondo. 
Pendekezo hilo lilitolewa kupitia timu mbalimbali toka wizarani, ofisi za kanda na halmshauri ya wilaya, ambazo zilitembelea kijijini hapo kuomba kupatiwa muhtasari wa kikao cha kijiji kitakachopitisha ombi hilo la serikali. Ombi hilo linakuja kwa kijiji kwa sababu msitu huo umekuwa
chini ya usimamizi wa wananchi wa kata ya Enguserosambu kwa miaka mingi. Ni wananchi hao ndio ambao wameutunza msitu huo pasipo Kuombwa wala Kukabidhiwa  na serikali. Na kwa kweli wameweza kuutunza kwa muda wote huo. Miti haijakatwa, wananchi wamejiwekea sheria ndogondogo na pia kuwakamata wale ambao wamekuwa wakiharibu msitu huo. Hivyo wananchi hawa wamewajibika katika kuhakikisha msitu unabaki katika hali yake ya asili pasipo kushurutishwa na mtu yeyote. 
Kwa mantiki hiyo muhtsari uliokuwa unaombwa na serikali ya
halmashauri yan wilaya ulihiitaji baraka za wananchi, ambao hawakuwa tayari kutoa sehemu ya uhai wao unaotegemea msitu huo. Hakuna mwanakijiji aliyekuwa tayari
kukubali ombi hilo. Na jibu lilikuwa ni wazi kabisa kwamba ombi hilo lilitishia
mustakabali wa jamii zinazozunguka msitu huo ambazo ni vijiji vya Enguserosambu,
Ng’arua, Orkiu na Naan.  Hivyo wakati
serikali ikipendekeza kuusimamia
msitu huo wananchi kwa upande mwingine wakaanza kuiomba
serikali iwaruhusu kuusimamia. Ni kama kichekesho pande zote zinaombana
kuusimamia msitu huo. Serikalikupitia halmashauri ya wilaya inasema tunahitaji kuusimamia,
na wananchi wanaiomba serikali hiyo hiyo kuusimamia msitu huo. “Kwa kweli sisi
kama wananchi wa Enguserosambu tumeona kwamba huu msitu ukiondoka chini ya
usimamizi wetu tutaathirika. Kwa sababu msitu huu ni uhai wa wananchi wa hapa.
Tukikosa huu msitu, hatupati maji wala mvua, tutakosa chakula. Kwa kifupi
tutakosa kitu muhimu cha uhai wa jamii,” anaelezea mraghbishi Noorkiyengop
Mbaima.
 Ndani ya msitu huu
kuna miti ambayo wazee wanaitumia kwa ajili ya shughuli za kimila pamoja na
miti ya kiasili ambayo inatumika kwa shughuli mbalimbali. Baadhi ya miti hiyo
ni pamoja na Oroilieni ambao unatumika kwenye shughuli za jadi, ujenzi na
kiimani. Akifafanua kuhusu mti huo Robert Kamakia anaelezea, “Huwezi kuingia
jando bila kuwa na mti Oroilieni. Kwa kuwa unatumika katika kufanya baadhi ya
shughuli za kimila. Mti mwingine ni Orikienyi ambao unatumika kama dawa ya
kutibia magonjwa ya aina mbalimbali kama homa, kifua, malaria na kadhalika. Mti
mwingine ni Ostiani ambao hutumika kwa ajili ya kivuli na kutunza maji.”  Hivyo msitu huu una maana kubwa sana kwa
makundi mbalimbali yakiwemo ya wazee, wanawake na vijana.  K wa upande wa vijana kwa mfano, mila na
desturi



za kimasai zinawataka kujitenga hasa  pale wanapoingia ngazi ya Morani. Ambapo hutakiwa
kuweka kambi kwa ajili ya kuchinja ng’ombe na kula nyama. Tukio hili huchukua mpaka
mwezi mmoja wakati vijana hao, wanapoazimisha sherehe hizo. Tukio hili
linashirikisha matumizi ya miti mbalimbali kwa mujibu wa taratibu zao. Supu
wanazokunywa huchanganywa na baadhi ya majani ya miti hiyo. Ni dhahiri ulaji wa
nyama kwa mwezi mzima unahitaji pia matumizi ya dawa za asili. Na ndio maana
wamasai hawasumbuliwi sana na magonjwa yanayotokana na ulaji
mwingi wa nyamba. Si hivyo tu porini hamna vitanda hivyo
baadhi ya majani hutumika kwa ajili ya zoezi hilo.   “Kiukweli bila msitu vijana hawawezi kufanya
chochote. Kwa kuwa kila kitu kinatoka katika huo msitu,” anafafanua Julius Long’oli.
Lakini si hivyo tu, wakati wanaingizwa jando pia kuna
miti inayotumika. Vivyo hivyo na katika sherehe za kumaliza jando. Hivyo msitu
ni sehemu ya mila na utamaduni wa jamii hizi zinaouzunguka. Ni imani yao pia,
ambayo kimsingi ni lazima iheshimiwe. Huu ni msitu wao wa enzi na enzi.  “Huu ni msitu wa jamii kwa Kimasai unaitwa
Elieteti yaani ndani ya jamii kwa maana ya jina hilo ni msitu unaosaidia jamii ya
sasa na ya kizazi kijacho. Kwamba huu msitu unategemewa na kizazi cha sasa na kijacho,”
anafafanua Yohana Tuluni mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya kusimamia msitu.  Mtizamo huu wa wananchi wa kata hii, kwamba
wao ndio wausimamie msitu huu, unatokana hali halisi ya msitu namba moja wa
Loliondo unaosimamiwa na serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro
kuwa katika hali ya kutoridhisha. Miti mingi  imekatwa kwa ajili ya matumizi ya ujenzi na hivyo
kutishia uhai wa msitu huo. Kitu ambacho wana Enguserosambu hawakupenda kitokee
kwa msitu namba mbili wa Loliondo ambao wanautegemea kwa mustakabali wa maisha
yao.  Msitu huu umekuwa ukitegemewa na
jamii ya hapa kwa miaka mingi. Ni wao ndio ambao wamekuwa wakiutunza na kwa kweli
wamefanikiwa kwa njia moja ama nyingine kuufanya uwe mzuri zaidi kuliko hata ule
wa Liliondo moja unasimamiwa na serikali.


“Wazo la kutaka kumiliki msitu lilikuwa kama ndoto,
ukiangalia na hali halisi ilivyokuwa. Ni maono ya mtu mmoja aliyewashirikisha wenzake.
Mwishowe wazo likatolewa Kwa wanakijiji ambao waliungamkono wazo hilo. Na
mwishowe tukamwandikia Mkuu wa Wilaya na kwa kweli alituunga mkono sana,” anafafanua
mraghbishi na mjumbe wa Bodi ya Wadhamini Jackso Nangiria   Mchakato wa kuomba hadi kukabidhiwa usimamizi
wa msitu umewezesha wananchi wa Enguserosambu kuongeza ufahamu wa mambo
mbalimbali juu ya usimamizi wa misitu lakini pia mahusiano baina ya wananchi na
viongozi yameboreka zaidi.  Umoja ni nguvu
utengano ni udhaifu, hivi ndivyo unavyoweza kusema Wanaenguserosambu wamekuwa
wamoja zaidi. Mashirika rafiki yamesaidia sana katika kutoa elimu kwa wananchi
na viongozi wao ambao maarifa hayo yamewezesha kujiwekea mikakati na hatimaye
kufanikisha jamii kumiliki msitu wake wa enzi kwenye mikono yake. Wakati
mchakato unaanza palikuwa na kijiji kimoja tu cha Enguserosambu kilichokuwa kinaundwa
na vitongoji vinne vya Enguserosambu, Ng’arua, Orkiu na Naan ambavyo sasa
vimepata hadhi ya kuwa vijiji. Kwa sasa sauti yao ni kubwa zaidi kuliko pale Mwanzo

 



Hivyo Bodi ya Wadhamini ilichaguliwa na mkutano mkuu wa
kijiji, ambacho sasa kina hadhi ya kata. Kwa hiyo usimamizi wa msitu huu kwa
sasa umekabidhiwa kwa Kata ya Enguserosambu.   Hivyo
wananchi kutoka katika kila kijiji walichagua wawakilishi wao waliounda Bodi ya
Wadhamini. Wawakilishi hawa jukumu lao kubwa ni kuratibu mchakato wote wa
uombaji usimamizi wa msitu wa Loliondo 2. Baada ya kuchaguliwa wajumbe walipatiwa
mafunzo na shirika la PALISEP ambao pia walisaidia uandikishwaji wa bodi tarehe
12/09/2012. Bodi hiyo imeundwa na wajumbe 10 kati ya hao wanawake ni 4.   Bodi
hii ilipata mafunzo ya sheria mbalimbali za misitu, usimamizi wa misitu na bodi
yenyewe pia kupitia video ya hali ya msitu wa Loliondo 1. Walipata pia ziara za
mafunzo kwa kutembelea misitu inayosimamiwa na jamii kwa mfano msitu wa Suledo
uliopo Manyara wilaya ya Kiteto. Bila jamii kujitoa kwa hali na mali
isingewezekana kufanikiwa kwenye hili. Kwani bodi ya wadhamini imefanya kazi
kubwa. Jamii imeshiriki katika kuandika katiba ya bodi na sheria ndogondogo ambazo
zimepitishwa katika mikutano ya vijiji.

 

“Baada ya kuchaguliwa jukumu letu ilikuwa ni kutembelea
msitu ili kujua hali yake. Lakini pia tuliweza kutoa elimu kwa wale waliokuwa
wanaishi na kufanya shughuli za kilimo ndani ya msitu. Ili waweze kuondoka. Si
kazi rahisi,” mjumbe wa Kamati ya Bodi ya Wadhamini Sunde Tutayo.





Kwa sasa mpango ni kuboresha na kutunza vyanzo vya maji.
Kupitia bodi hiyo, wananchi wamejiwekea malengo ya kuuongeza zaidi kwa kupanda miti
zaidi. Hili linafanywa kwa uangalifu mkubwa kwa kuwa kuna baadhi ya miti si
rafiki mzuri kwa vyanzo vya maji inayakausha.  Lakini si hivyo tu Bodi ya Wadhamini
inaangalia njia sahii ya kuhakikisha kwamba zinapatika fedha za kununulia miti
mipya. Wazo lililopo ni kuwakilisha mtizamo huu kwa wanajamii ili waweze kutaarifiwa
na kusikilizwa nini yatakuwa maamuzi yao kwenye uchangishaji huo wa fedha.   Changamoto nyingine ni uboreshwaji wa sheria
ndogondogo kwa kuwa hakuna mipaka ya majukumu baina ya Bodi ya Wadhamini na
Halmashauri ya serikali za vijiji. Kuna umuhimu wa suala hili kuwekewa utaratibu
mzuri wa kiuwajibikaji kwa sababu muda mwingine vyombo hivi vinaweza kugongana
kimawazo na kiutendaji na nani anawajibika kwa nani.





“Hapo nje kuna mikaratusi tumeikamata sisi kama Bodi ya
Wadhamini. Mtu ameangusha mti mbichi ambao haujakauka. Na ameiyangusha bila idhini.
Tumefanya hivi kwa kushirikiana na Mheshimiwa Diwani. Tunachosubili tukae na
serikali ya kijiji ili tujue tunafanya nini,” anafafanua mraghbishi na Kaimu
Katibu wa Bodi ya Wadhamini Jackson Nangiria.   Kwenye
kukabidhiwa msitu mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya na Diwani wa Kata ya Enguserosambu
walikuwepo wakati wa kukabidhiwa kwa msitu huo pamoja na wenyeviti wa vijiji
vyote vinavyounda kata ya Enguserosambu.  Kwa hakika wenzetu wa Enguserosambu wameweza
kujipanga na kuhakikisha kwamba msitu wao wa enzi unabaki mikononi mwao.