Barrick yatumia bilioni 1/- kutengeneza barabara za Tarime

Nembo ya Barrick

Mwandishi Wetu
Tarime

MGODI wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya Barrick umetumia zaidi ya shilingi bilion 1 katika kipindi cha hivi karibuni kukarabati barabara muhimu kwenye wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Katika mchango wake wa hivi karibuni, Barrick imetoa msaada wa shilingi milioni 600 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa ajili ya ukarabati wa barababara ya zamani ya Wajerumani iliyopo kwenye eneo hilo.

Msaada huo uliotolewa na mgodi wa North Mara unakuja wakati kampuni hiyo tayari ilikwishawekeza dola za Marekani $340,000 (sawa na zaidi ya shilingi milioni 500) kwenye kufanya ukarabati kwa barabara hiyo mwaka 2007.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 45 ni moja kati ya miundombinu muhimu sana kwenye eneo hilo ambayo inawaunganisha maelfu ya wakazi wa wilaya hiyo kwenye barabara ya lami ya Mwanza-Sirari.

Barabara hiyo ni kiungo muhimu kati ya eneo la Nyamongo na mji wa Tarime uliopo mkoa wa Mara. Mpaka kufikia sasa hivi, kampuni ya Barrick imeshawekeza zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kukarabati barabara za wilaya ya Tarime kuhakikisha kuwa zinapitika mwaka mzima.

Barrick imesema kuwa imeamua kutoa mchango wake kuimarisha miundombinu ya wilaya ya Tarime ili kufungua fursa nyingi zaidi za maendeleo na huduma kwa jamii kuwafikia wakazi wa vijiji viliopo kwenye wilaya hiyo.

Mgodi wa North Mara pia ulifanya ukarabati wa barabara kwenye vijiji vya Kewanja, Nyangoto na Matongo katika jitihada zake za kutoa mchango kwenye shuhuli za maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo.

Vijiji hivi ni miongoni mwa vijiji saba vinavyozunguka mgodi huo ambapo Barrick imewekeza kwenye miradi ya elimu, maji. umeme wa vijijini na barabara ili kuwawezesha wanavijiji wapate maendeleo bora.

Maofisa kutoka mgodi huo wamesema kuwa lengo la Barrick ni kutoa msaada kwa jamii zote zinazozunguka migodi yake pamoja na maeneo mengine ya Tanzania. Misaada mbalimbali inayotolewa na Barrick imewezesha mgodi wa North Mara kuweza kuboresha mahusiano yake na wanakijiji wa eneo hilo.

Mgodi wa North Mara umekuwa unafanya kazi kwa karibu na serikali pamoja na wananchi wanaoishi eneo karibu na mgodi huo katika kufanya uamuzi wa vipaumbele vya miradi ambayo kampuni hiyo inaweza kuifadhili ili kuleta maendeleo kwa wananchi.