Japani Yaipa Tanzania Bil 210 Kusaidia Nishati ya Umeme
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba na Serikali ya Japani kiasi cha shilingi Bilioni 210 kwa ajili ya maendeleo ya mradi wa njia ya kusafirishia umeme kati ya Tanzania na Kenya ambao utasaidia upatikanaji wa umeme wa kutosha.
Mkataba huo wa masharti nafuu ulisaininiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dk. Servacius Likwelile na Balozi wa Japani nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusaini mkataba huo Dkt. Likwelile alisema kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika kusambaza nyaya za umeme zenye KV400, na urefu wa kilometa 414.5 kati ya Singida na Namanga kupitia Babati na Arusha.
Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea maendeleo ya jamii na uchumi nchini kwa kuleta muungano wa kibiashara katika nchi za Afrika Mashariki.
Naye Balozi wa Japani nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida alisema kuwa mkopo huo utafanikisha kusambaza nyanya za umeme zenye urefu wa takribani kilometa 508 kati ya Tanzania na Kenya ambapo Tanzania itasambaza kilometa 415 wakati Kenya itakuwa na kilometa 93.
Japani imekuwa ikisaidia Tanzania katika miradi ya umeme kwa muda mrefu, miradi ambayo tayari imekamilika ni pamoja na usambazaji umeme Zanzibar, mradi wa usambazaji nyaya za umeme mkoani Kilimanjaro na mradi wa kutengeneza nyaya mpya za umeme jijini Dar es Saalam.