Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Atoa Mwelekeo wa Utendaji Wake

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ujenzi pamoja na Taasisi zake kuhusu ufanyaji kazi kwa uadilifu kwa kuzingatia maslahi ya jamii.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ujenzi pamoja na Taasisi zake kuhusu ufanyaji kazi kwa uadilifu kwa kuzingatia maslahi ya jamii.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa watendaji wa Wizara hiyo namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili na mikataba wanayoingia iwe kwa maslahi ya nchi.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa watendaji wa Wizara hiyo namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili na mikataba wanayoingia iwe kwa maslahi ya nchi.


NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amewataka watumishi wa Wizara mpya ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufanya kazi kwa ubunifu kwa kuzingatia matokeo chanya na kuachana na hulka ya kufanya kazi kwa mazoea.
Akizungumza na viongozi wa Wizara hiyo mpya, Eng. Ngonyani amesisitiza umuhimu wa watendaji na watumishi kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuzingatia maslahi ya jamii ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
“Tuwe tayari kubadilika, tufanye kazi ya kuwahudumia watanzania kwa moyo, tusifanye kazi kwa mazoea na kuzoea matatizo na asiyeweza atupishe”, amesisitiza Eng. Ngonyani.
Ameuagiza Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kuongeza ubunifu na kuhakikisha katika kipindi kifupi kuanzia sasa magari yote ya Serikali yanatengenezwa katika karakana zake.
Aidha, Eng. Ngonyani amewataka TEMESA kuongeza wataalamu katika karakana zake ili kuvutia magari binafsi kutengenezwa katika karakana hizo na hivyo kujijengea uwezo wa kitaalam na kiuchumi.
Kuhusu Changamoto zinazoikabili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Nyerere na Shirika la Reli Tanzania (TRL) amewataka watendaji wa taasisi hizo kuhakikisha wanaingia mikataba yenye maslahi kwa nchi, kuisimamia kikamilifu mikataba hiyo na kuachana na mikataba yenye manufaa binafsi ambayo huzalisha bidhaa mbovu na huduma zisizokidhi viwango.
Kuhusu Sekta ya Mawasiliano, Naibu Waziri Eng. Ngonyani, ameipongeza sekta hiyo kwa kuboresha mawasiliano nchini na kusisitiza kasi katika mchakato wa ujenzi wa mkongo wa taifa ili uweze kunufaisha sekta ya elimu na afya kwa haraka zaidi.
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unajengwa kwa Awamu ambapo Awamu ya I na II zimekamilika na Mkongo huo unatumiwa na Makampuni ya Simu, mabenki, shule, hospitali na Serikali kwa kutumia huduma ya Mtandao na Awamu ya III inaendelea ambapo Mkongo huo umeunganishwa na Nchi jirani sita za Kenya, Uganda, Zambia, Malawi, Rwanda na Msumbiji na Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya.
Aidha, Mhe. Ngonyani ameyataka Makampuni ya Simu nchini kujisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam ili wananchi wawe na hisa na kumiliki makampuni ya simu kwa kuwa tayari kanuni husika iko tayari na imetangazwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 7 Agosti 2015 na kupatiwa Na. 219. Aliongeza kuwa,
“Haiwezekani kitu kikubwa kama Kampuni za Simu zisimilikiwe na wananchi wakati Bunge lilidhamiria wananchi wawe na Hisa na kumiliki makampuni hayo” .
Takribani Dola za kimarekani milioni 263 zimetumika katika ujenzi wa mradi wa mkongo wa taifa unaotarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 403 utakapokamilika.
Kikao hicho cha kumkaribisha Naibu huyo kimehudhuriwa na Wakuu wa taasisi na vitengo vya iliyokuwa Wizara ya Ujenzi; Uchukuzi na Mawasilino, Sayansi na Teknolojia, wakiongozwa na makatibu wakuu Eng. Mussa Iyombe na Yamungu Kayandabila.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.