SHIRIKISHO la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph kwa kumteua Dk. Abdallah Possy kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, kazi, Ajira, Bunge, Vijana na Walemavu). Dk. Possy ambaye pia ni ambaye ni Mwalimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma, ameteuliwa kuwa mbunge na Naibu Waziri katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa shirikisho hilo Amon Mpanju alisema wanaishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kutimiza ahadi yake ya kuwajali na kuwapa kipaumbele jamii ya watu wenye ulemavu kwa kuhamisha usimamizi wa masuala ya watu wenye ulemavu toka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kuyaweka chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa utekelezaji wenye tija chini ya Serikali yake.
“Ni Faraja kwetu Watanzania hususani sisi wenye ulemavu tumetengewa nafasi yetu maalum ndani ya Serikali hatua ambayo itaifanya Serikali kutenga rasilimali za kutosha ili kuwezesha utekelezaji wa masuala yetu,” alisema Mpanju.
Aidha Bwana Mpanju aliiomba Serikali kushughulikia changamoto zao ikiwa ni pamoja na kuifanyia marekebisho ya Sheria ya Haki za Watu wenye Walemavu ili iakisi muundo mpya wa uratibu na usimamizi wa masuala ya watu wenye ulemavu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mpanju alisema wameiomba Ofisi ya Waziri Wkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Ofisi ya Bunge Ikulu kuajiri wakalimani wa lugha ya alama ambao watakuwa watafanya tafsiri ya mijadala ya vikao vya Bunge, Hotuba za Rais na taarifa za habari na vipindi vyote muhimu vinavyotolewa kwa umma kupitia runinga.
Kwa mujibu wa Mpanju alisema Shivyawata pia limeiomba Serikali kuhakikisha kuwa vyuo vya ufundi vilivyo chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii ambavyo vilikuwa vinatoa ujuzi kwa watanzania wenye vinafufuliwa na vihamishiwe Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknoloia na Ufundi.
Mpanju aliwataka Watanzania wamuunge mkono, Dk. John Pombe Magufuli na Serikali ya awamu ya tano katika kuzishughulikia kero zinazoikabili nchi yetu na kikubwa kumuombea kwa mungu ili amtunze na kumwezesha kuyatimiza malengo yake.