Na Mwandishi Wetu, Igunga
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kilikuwa mstari wa mbele katika maandalizi na mazishi ya Peter Ezekiel (12) aliyegongwa na lori mjini hapa juzi. Ezekiel alikufa papo hapo baada ya kugongwa na lori la mizigo lililokuwa likitokea Nzega kwenda Singida, alipojaribu kukatiza barabara akitokea katika umati wa wananchi waliokuwa wakisubiri msafara wa mgombea ubunge Jimbo la Igunga kwa tiketi ya CCM, Dk. Peter Kafumu.
Dk. Kafumu na msafara wake akiwemo mratibu wa kampeni za CCM jimboni humo, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba walikuwa wanatokea Singa kwenda kuchukua fomu kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga.
Baada ya mtoto huyo kugongwa na kufariki papo hapo mgombea huyo na msafara wake waliamua kusitisha kwa muda kazi aliyokuwa amefuata ya kuchukua fomu hizo na badala yake wakashiriki kuuchukua mwili kutoka eneo la tukioo kuupeleka hospitali.
Katika mazishi mgombea wa CCM, Viongozi wote wa CCM na wilaya ya Igunga na kundi kubwa la wanachama walishiriki tangu kuandaa mazishi ikiwemo kununua sanduku la kuhifadhia mwili hadi kuupeleka mazikoni.
“Tumefarijika kwamba tumeshiriki kikamilifu mazishi ya mtoto wetu kama tulivyoahidi jana (juzi) ulipotokea mkasa huu, hatukufanya hivi kujipendkeza lakini imetuwia kwa sababu za kibinadamu na pia ni mtoto ambaye ni miongoni mwa familia zilizopo katika jimbo hili ana kikubwa zaidi licha ya CCM kutohusika kusababisha kifo hiki lakini tunaamini alikuwa miongoni mwa mashabiki wetu, maana chama hiki ni cha wazee, vijana na watoto,” alisema Nchema katika mazishi hayo.
Naye Kulwa Mpina ambaye ni mama mdogo wa marehemu, aliyekuwa katika mazishi hayo yaliyofanyika katika makaburi yaliyopo nje kidogo ya mji wa Igunga, alisema wamefarijika sana na hatua iliyochukuliwa na CCM kusaidia katika msiba huo mzito.
“Kwa kweli sisi familia yetu tutampigia kura mgombea wa CCM ili ashinde katika uchaguzi huu na kuwa kumbukumbu ya marehemu mtoto wetu,” alisema huku akibubujikwa machozi.
“Tunajua CCM haikuhusika kwa vyovyote na kifo hiki, lakini imeamua kuchukua jukumu la kuwa karibu nasi kwa sababu mbali na kwamba tulikuwa naye katika kusubiri msafara wa mgombea lakini sisi na mtoto huyu ni wakazi wa jimbo hili”, alisema Kashinde Raphael aliyejitambulisha kuwa ni mwanafamilia ya marehemu. Katika msiba huo CCM Taifa imetoa rambi rambi ya Sh. milioni moja huku Chadema Taifa ikitoa Sh. laki moja na wilaya sh. 20,000.
Viongozi wa kitaifa kwa CCM alikuwepo Katibu wa NEC Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba na kwa CHADEMA alikuwepo Mwita Mwikwabe ambaye ndiye mratibu wa Kampeni za Chadema jimboni Igunga.
Katika uchaguzi mdogo jimbo la Igunga CCM imemsimamisha Dk. Kafumu kugombea katika uchaguzi huo ambao unafanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Rostam Aziz (CCM) baada ya kujiuzulu. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu baada ya kampeni zitakazorindima kwa wiki kadhaa baada ya kuanza rasmi Septemba 7, mwaka huu.