ACT Wazalendo Kuandamana Kumponge Rais Magufuli…!

ACT Wazalendo

ACT Wazalendo

JANA arehe 10/12/2015 Uongozi wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar Es Salaam umemuandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, kumuomba apokee maandamano yetu ya amani siku ya Jumatano tarehe 16/12/2015 yatakayoanzia ofisi za ACT-Wazalendo Mkoa yaliyopo Keko Maduka Mawili na kuishia ofisi ya Mkuu wa Mkoa (Ilala Boma).

Lengo la maandamano;-
Maandamano yetu hayo yana malengo makuu matatu
1-Kuunga mkono vita dhidi ya Ufisadi na Rushwa inayopiganwa na Rais Dk John Magufuli,ikiwa ni pamoja nadhamira ya wazi ya kusimamia ukusanyaji kodi Kama inavyosema katika ilani ya ACT-Wazalendo ya mwaka 2015 ukurasa wa 36 na 37.

2.Kumtaka Rais asimamie Uongozi bora wenye lengo la kurudisha nchi kwenye misingi iliyoasisiwa na wazee wetu hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume.
Tunafanya hivi tukiwa na kumbu kumbu nzuri ya ilani yetu ya uchaguzi ya Mwaka 2015 katika ukurasa wa saba inayoelezea kuwa Ndoto ya ACT-Wazalendo ni kuona “Taifa lenye kujitegemea kiuchumi na kiutamaduni, na ambalo linalinda na kudumisha usawa, ustawi wa jamii, uwajibikaji, Demokrasia na uongozi bora”.
Pia tukiwa na imani ya kwamba mambo hayo yatatekelezwa vizuri kwa nchi kujiwekea miiko ya uongozi kama inavyoelezwa na Azimio la Tabora lililohuishwa kutoka katika Azimio la Arusha

3 Lengo letu la mwisho katika maandamano hayo ni Kumuomba Rais ahakikishe nchi kupitia mamlaka husika inasimamia mfumo wetu wa katika Fedha Kama inavyosema katika ilani ya ACT-Wazalendo ukurasa wa 23
“Hata hivyo, yote haya hayatakuwa na maana iwapo mfumo wa fedha kupitia mabenki utakuwa umeshikwa na wageni, Nchi yetu haiwezi kuendelea iwapo mabenki makubwa yote yatakuwa yamebinafsishwa
Uanzishaji wa mabenki uliofanyika mwaka 1967 na kuundwa kwa Benki ya Taifa ya Biashara,(NBC), Benki ya Nyumba na Benki ya Maendeleo Vijijini ilikuwa ni maamuzi ya msingi sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara ni maamuzi ya hovyo kabisa kupata kutokea katika historia ya nchi yetu”.

Kwa sababu ya maandamano hayo pia uongozi wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar Es Salaam umeandika barua kwenda Polisi Kanda Maalum kwa ajili ya kuwapa taarifa ya maandamano hayo ya Amani ya tarehe 16/12/2015 kwa ajili ya kupata ulinzi.

ACT-Wazalendo, Taifa Kwanza Leo na Kesho

………………………..
Eng.Mohamed. M Ngulangwa,
Katibu wa ACT-Wazalendo,
Mkoa wa Dar Es Salaam.