TGNP Kuonesha Filamu za Ukatili Mitaani

Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia

Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia


KATIKA kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mwaka huu, TGNP Mtandao pamoja na shughuli nyingine, itaonesha filamu na makala za ukatili wa kijinisa katika vibanda vya kuonesha mpira na filamu katika mitaa mbalimbali katika jiji la Dar es salaam. Hii ni katika kuendelea kuifikia jamii katika njia raisi na rafiki zaidi na hivyo kufikisha ujumbe uliokusudiwa. Ikumbukwe kuwa baadhi ya vibanda hivyo vimekuwa sehemu ambazo filamu zinazochochea ukatili wa kijinsia huoneshwa. Mitaa itakayonufaika na mkakati huo ni pamoja na Mwananyamala, Kipunguni, Kigogo, Mabibo na Mbagala.

UMUHIMU WA KUMLINDA MTOTO ILI APATE ELIMU
Kama tathmini ya Malengo ya Milenia ilivyofanyika na jumuiya za kimataifa tangu utekelezaji wake ulivyoanza mwaka 2000, ndivyo malengo ya maendeleo endelevu yanavyowekwa ili kutekelezwa hadi mwaka 2030. Hivyo, ni muda mwafaka wa kutizama matokeo/athari za hatua/juhudi za kijamii, kiuchumi na kisiasa katika kuwalinda watoto hasa watoto wa kike ili kupambana na umasikini, ukatili, kutengwa na ubaguzi na kufikia usawa na maendeleo endelevu.

Elimu ni haki ya msingi inayotambuliwa na Ibara ya 26 ya Tamko la Umoja wa Mataifa la haki za Binaadamu la mwaka 1948 na kusisitizwa katika makubaliano na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa. Kadhalika, Mkakati wa Kupambana na Kuondoa Umasikini Tanzania (MKUKUTA) unalenga kuleta usawa katika kupata elimu bora ya sekondari kwa wavulana na wasichana na kupanua elimu ya juu, elimu ya ufundi na elimu ya mafunzo. Pia sera ya Elimu inayolenga kutatua changamoto hizo kupitia ujenzi wa mabweni, kukabiliana na mimba za utotoni, upatikanaji wa huduma ya maji na nishati ya umeme mashuleni na kuweka mazingira wezeshi kwa mtoto wa kike.

Pia Sheria ya Mtoto inaainisha haki za mtoto ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, utu, heshima, uhuru, afya, elimu na hifadhi kutoka kwa wazazi. Licha ya hayo, bado mtoto wa kitanzania anakabiliwa na changamoto zinazomsababisha kupata elimu. Moja kati ya changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa shule na waalimu, wazazi kushindwa kumudu gharama za shule ikiwemo ada. Kadhalika baadhi ya maendeo watoto wanazimika kusafiri umbali mrefu kwenda shule, wazazi/walezi kulazimisha watoto kuolewa, wanafunzi kushindwa kusoma kutokana na ukosefu wa nishati kwaajili ya mwanga ili kusoma hasa nyakati za usiku.

Pamoja na changamotio hizo zinazomkabili mtoto, kwa ujumla, mtoto wa kike amekuwa hafaidi haki yake ya elimu kwa kiasi kukubwa kwa kuzingatia pamoja na mambo mengine, maumbile yake kibaiolojia ambapo baadhi yao hulazimika kukosa masomo siki 3-7 kila mwezi, mila na desturi zinazomtwisha majukumu ya kifamiliya, sherai kandamizi kama Sheria ya Ndoa ya mwak 1971 na sheria nyinginezo.

Kuna idadi kubwa ya wanafunzi huacha masomo/shule nchini Tanzania huku wasichana wakiwa wengi zaidi ya wavulana. Ni asilimia 65.3 pekee ya wanafunzi wanaoandikishwa huhitimu elimu ya msingi nchini. Takwimu pia zinaonesha kuwa, asilimia 37 ya wasichana huolewa kabla ya kufikia miaka 18 hali inayoendeleza kokosekana kwa usawa wa kijinsia hivyo kurudisha nyuma haki za wanawake. Licha ya kuwa idadi ya watoto wanaoolewa imepungua, idadi ya wasichana wanaoolewa bado ni kubwa. Mikoa inaayoongoza kwa ndoa za utotoni ni pamoja na Manyara,(71%), Dodoma, (64%), Arusha, (59%), Shinyanga 59%, Tabora 58% na asilimia 55 mkoa wa Mara huku mikoa yenye idadi ndogo ikiwa ni Dar es salaa 8% na Iringa 17%, (TDHS 2010).

Vitendo vya Ukatili wa kijinsia inaathiri wavulana na wasichna kama inavyooneshwa katika utafiti wa Taifa kuhusu Ukatili dhidi ya watoto (2009). Utafiti huo unakisia kuwa kufikia miaka 18, asilimia 28% ya wasichana ambayo ni zaidi ya robo na asilimia 10 ya wavulana wanafaniwa ukatili wa kingono hasa nyumbani. Karibia robo tatu (73% wasichna na 72% wavulana) walishafanyiwa ukatili wa kimwili kama vile vipigo (kupigwa vibao, mateke na kuchapwa viboko)._Asilimia 60 ya vitendo hivyo vilitekelezwa na ndugu. Asilimia 21.6 ya wavulana na asilimia 17.7 walifanyiwa ukatili wa kisaikolojia.
TGNP INAFANYA NINI?
Katika kuadhimisha siku 16 mwaka huu, TGNP kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inafanya yafuatayo;
i. Kuandaa mijadala ya wazi kuhusu ukatili wa kijinsia katika vituo vya taarifa na maarifa katika mikoa ya Shinyanga (Kishapu) na Mara (Tarime)
ii. Kuandaa na kuendesha warsha kuhusu mada mbalimbali za ukatili wa kijinsia ikiwemo rushwa ya ngono, nk ikilenga asasi za kiraia, wanafunzi wa vio na shule za msingi na sekondari, vijana na makundi mengine.
iii. Kuandaa na kuonesha filamu na makala mbalimbali kuhusu ukatili wa kijinsia katika vibanda vya kuonesha filamu katika mitaa mbalimbali katika jiji la Dar es salaam

WASHIRIKI
Shughuli hizo zinatarajiwa kushirikisha zaidi ya watu 800 ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa vyuo, vyuo vikuu, shule za sekondari na msingi, asasi za kiraia na kidini, waandishi wa habari, taasisi mbalimbali za kiserikali, wadau wa maendeleo, vijana, washiriki wa semina za maendeleo na jinsia, vituo vya taarifa na maarifa pamoja na wananchi kwa ujumla.

Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia huadhimishwa kimataifa kuanzia tarehe 25/11 hadi tarehe 10/12 kila mwaka. Ndani ya siku hizi 16 kuna matukio yanayofanyika yakilenga kutetea haki za binaadamu. Tarehe 25/11 ni siku ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake, 29/11 ni siku ya watetezi wa haki za wanawake, 1/12 ni siku ya ukimwi duniani, 3/12 siku ya watu wenye ulemavu duniani, 6/12 kumbukumbu ya mauaji ya kikatili ya wanawake 14 wa Motreal na 10/12 ni siku ya haki za binadamu duniani.

Lengo kuu la siku hizi 16 ni kuendeleza mijadala, kutafakari kwa pamoja kuhusu mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia, mafanikio yake, changamoto na namna ya kujipanga na kusonga mbele kwa pamoja. Kauli mbiu ya kitaifa mwaka huu “Funguka! Chukua Hatua, Mlinde Mtoto Apate Elimu” Hii ina maana kuwa tuvunje ukimya kila tunaposhuhudia kitendo chochote cha ukatili wa kijinsia, tuchukue hatua katika nafasi zetu tofautitofauti ili tuwalinde watoto waweze kunufaika na elimu katika nchi yetu. Walengwa hasa ni watoto wa kike na wa kiume pamoja na wanawake kwa ujumla ambao ndio wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia kwa namna mbalimbali.