Shibuda ajichimbia kaburi lake

 

Na Sophia Yamola

GAZETI la Chama Cha Mapinduzi (CCM) lilipoandika wiki iliyopita kwamba Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda “amejilipua” lilijua linachokifanya.

Ilikuwa baada ya mbunge huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwashutumu viongozi wake kwa mafumbo, na hata kuwafananisha na Nduli Idi Amin wa Uganda.

Inashangaza Shibuda amekuwa anatumia fursa ya kuchangia bungeni kukishutumu chama chake hadharani. Kumbukumbu zinaonyesha tangu amechaguliwa kuwa mbunge wa CHADEMA mwaka jana, Shibuda ametofautiana hadharani na viongozi wake mara tatu.

Mara ya kwanza ilikuwa katika kikao cha kwanza cha Bunge, pale wenzake waliposusia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete bungeni, na kukataa kushiriki shughuli zake hadi hapo atakapojibu hoja za msingi, ikiwamo umuhimu wa mabadiliko ya katiba.

Wabunge wa CHADEMA waliokuwa bungeni, walinyanyuka na kuondoka mara tu Rais Kikwete alipoanza kuhutubia. Wachache kwa udhuru waliotoa, hawakuingia hata bungeni. Sidhani kama Shibuda alitoa udhuru wowote, lakini hakuonekana bungeni. Jioni alionekana akisamiliana na Rais Kikwete katika hafla iliyoandaliwa na rais kwa wabunge hao, Ikulu Chamwino.

Baadaye alipopata fursa ya kuchangia bungeni, badala ya kujielekeza kwenye hoja iliyokuwa mbele yake, aliwashambulia viongozi wa CHADEMA, akisema wenzake ni wanaharakati, na kwamba yeye ndiye mwanasiasa mahiri.

Mara ya pili ilikuwa katika kikao hiki cha Bunge, alipotofautiana na wabunge wenzake katika msimamo wa kususia posho. CHADEMA kimekuwa kinasisitiza kwamba posho za vikao kwa watumishi wa umma, wakiwamo wabunge, ni matumizi mabaya ya fedha za umma; na kwamba pesa hizo zingefaa zielekezwe kwenye kuinua kipato cha watumishi wa chini.

Alipopata fursa ya kuchangia hotuba ya waziri mkuu, Shibuda aliwashutumu wenzake, akidai hata posho yenyewe wanayopewa haitoshi. Akataka Bunge liwaongezee posho hiyo hadi Sh 500,000 (laki tano).

Alidai wanaokataa posho hizo wana pesa, na kwamba wabunge maskini kama yeye wanazihitaji kwa ajili ya misiba, harusi na kadhalika. Akawaita wenzake “wabunge maslahi binafsi,” na kwamba yeye ni “mbunge maslahi ya jamii.”

Mara ya tatu ni wiki iliyopita, alipowashambuliwa kwa mafumbo na kuwafananisha viongozi wake na Idi Amini.

Zipo habari pia kwamba wabunge wa CHADEMA walipokuwa kwenye vikao vya ndani vya kuwekana sawa na kupanga mikakati ya kazi, mwanzoni mwa mwaka, Shibuda aliwarukia kwa maneno makali na kuwashambulia kwamba hawajui siasa, ni watoto wachanga na wanaharakati.

Wabunge walimjia juu mmoja baada ya mwingine. Mbunge mmoja kijana akamwambia Shibuda, “kama umetumwa na CCM kuvuruga chama chetu, mlango ule pale. Rudi ulikotoka.”

Ndani ya chama na mbele ya umma, Shibuda amekuwa anapenda kujionyesha kama mwanasiasa mahiri, mzee wa busara, mkongwe mwenye busara za kisiasa ambazo “watoto wa CHADEMA wanapaswa kuvuna.”

Amekuwa akisema kwa rafiki zake kadhaa, ndani na nje ya vyombo vya habari, kwamba CHADEMA hawamheshimu wakati yeye ni mzee, na kwa makuzi aliyopewa, uzee ni dawa.

Lakini anasahau kwamba kama suala ni uzee, CHADEMA kinao wazee wengi, na hatuwasikii wakilalamikia uongozi wa vijana walionao. Hata pale yanapotokea matatizo ya kiutendaji au ya kinidhamu, wamekuwa wakihusika kutoa ushauri na kuchukua hatua bila kelele wala lawama hadharani.

Sana sana, wazee wa CHADEMA wamekuwa wanajivuna kuwa na timu ya vijana wachapakazi wanaokipa chama sura ya matumaini na uhai usioonekana katika vyama vingi tulivyo navyo.

Mbele ya macho ya wengi, Shibuda si mwana CHADEMA. Ni mwana CCM aliyevaa u-CHADEMA kupata ubunge. Na sasa anatumia ubunge wake kufyatua makombora dhidi ya CHADEMA.

Kinachoshangaza wengi pia ni upole wa Spika wa Bunge, linapofika suala la mbunge kuacha kujadili hoja iliyo mbele ya Bunge, akaanza ama kujitetea binafsi au kushambulia viongozi wa chama chake.

Hii inaongeza tetesi kwamba Shibuda anafanya kazi aliyotumwa. Lakini sasa kwa kasi hii atawafanya hata hao “waliomtuma” waone aibu kujihusisha naye, maana haifanyi kwa akili.

Wanaofuatilia mwenendo wa Shibuda wanasema kuwa makundi mengi ya watu anaoshinda nao, anaokunywa nao, anaobadilishana nao mawazo, na wanakiri kwamba haonekani kupenda kukaa na wana CHADEMA wenzake. Sana sana anatumia muda mrefu kuwasema vibaya na kuwapiga vijembe.

Tabia yake hiyo ndiyo ilimfanya Katibu wa Wabunge wa CHADEMA, John Mnyika kumshitaki kwenye chama, katika shauri ambalo hatujajua limefika hatua gani.

Lakini ni wazi kuwa Shibuda hana moyo wa kujisuta. Hatambui kasoro zake. Anatumia muda mrefu kujisifu, jinsi alivyo jabali la kisiasa, na jinsi alivyoshinda ubunge bila kampeni kubwa.

Anachosahau ni kwamba kama si CHADEMA, asingepata ubunge. CCM walishamtupa kwenye kura za maoni. Walishamchoka.

CHADEMA walimwokota kwenye jalala. Wakamteua. Wakampatia jukwaa, baadhi yao wakamchangia pesa, wengine wakaenda kumnusuru wakati alipokamatwa na kuwekwa ndani kwa kesi ya mauaji ya kubambikiwa siku chache kabla ya kupiga kura.

Mbunge wa Maswa Magharibi, Sylvester Kasulumbayi, ambaye wana Maswa walikuwa wakimwita Yesu, alifanya kampeni katika majimbo mawili – kwake na kwa Shibuda – wakati Shibuda akiwa katika matatizo.

Wana CCM wenyewe wanasema kwamba anachokifanya CHADEMA leo ndicho alikuwa akifanya kwenye CCM, lakini kwa kuwa kilikuwa chama tawala kulikuwa na uficho. Na wanasema ndiyo maana hata alipogombea vyeo ndani ya CCM hakupita.

Mara zote alilalama kwamba anaonewa, lakini wanachama wenzake wa zamani wanasema kuwa walishamjua kwamba ni tatizo, wakaamua kumnyima fursa za kuendelea kuwasumbua ndani ya vikao.

Ni dhahiri kwamba Shibuda anakihitaji CHADEMA kuliko chama hicho kinavyomhitaji. Anaweza kujitapa kwamba liwalo na liwe, lakini hawezi kuwa na uhakika kwamba akifukuzwa na CHADEMA leo, akahamia chama kingine, ataupata ubunge.

Shibuda ameshindwa kusoma alama za nyakati, hasa katika mazingira ambamo CHADEMA kimekuwa taasisi kubwa inayotikisha chama tawala, na inayoaminiwa na wananchi.

Tambo zake kuwa anapingana na viongozi maslahi ndani ya chama chake si kweli, kwani ameonyesha jinsi asivyo tayari kuacha posho ya kikao, ambayo chama chake kimesema ikiondolewa na kuhamishiwa kwengine itaboresha maisha ya watumishi wengine wasio na masilahi manono kama ya wabunge.

Baadhi ya wana CHADEMA na waandishi wa habari walio karibu na Shibuda wanasema kwamba uadui wa Shibuda na chama chake unatokana na ukweli kwamba alipohamia kwenye chama hicho mwaka jana, alidhani angepewa pesa ya kufanyia kampeni.

Mara kadhaa aliwaendea viongozi wa CHADEMA na kuwaomba wampe pesa, lakini majibu aliyopata yalimkatisha tamaa, kwani walimwambia yeye kama mbunge aliyemaliza ngwe yake, alipata kiinua mgongo.

Wakamweleza kuwa wabunge wote wa CHADEMA hawapewi pesa na chama; sana sana wao ndio wanapaswa kuchangia chama na kusaidia wagombea wasio na chochote. Baadhi ya viongozi aliowaomba pesa nao walikuwa wanagombea majimbo, wakamweleza kuwa nao wanazihitaji pesa hizo.

Kwa chuki na hasira alizotoka nazo hapo akajiapiza “kuwashughulikia” baadhi ya hao waliomnyima pesa. Wanasema Shibuda amekuwa pia anakerwa na kauli za viongozi za kuwataka wabunge wachangie chama kama njia ya kudumisha utamaduni wao uliokifikisha chama hapo kilipo.

“Anasema kama walikifikisha hapo kwa michango yao, ilikuwa ni uamuzi wao, wasijitape wala kuwalazimisha na wapya wachangie. Hii haikubaliki, na ni kielelezo kingine cha ubinafsi wa Shibuda,” anasema mwanachama mmoja kijana ambaye Shibuda amekuwa anamsimulia mikakati yake ya kuwashughulikia viongozi wake.

Baadhi ya wanachadema wanadhani kwamba Shibuda hajajua hata sera ya chama chake. Wanaamini hajui hata katiba na kanuni za chama zinasemaje; vinginevyo mambo anayofanya sasa yangepaswa kufanywa na “mgonjwa wa akili.”

Kwa hakika, hapa ambapo Shibuda amejifikisha, anaweza kuwa anajichimba kaburi lake mwenyewe.

Chanzo: Mwanahalisi