Tevez asema ataheshimu mkataba Man City

Mchezaji CARLOS Tevez

CARLOS Tevez amekiri itakuwa “vigumu” kuondoka Manchester City kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili msimu huu. Tevez alikuwa na matumaini angeondoka katika klabu hiyo ili aweze kuwa karibu na mabinti wake nchini Argentina. Lakini taarifa za karibu na mchezaji huyo zimeiambia BBC: “Itakuwa haiwezekani kwa Carlos kuondoka na hilo analifahamu.”

Ameongeza kusema klabu ya Inter Milan imemtaka mshambuliaji huyo, lakini imeshindwa na kiasi cha pesa walichoweka Manchester City. Kubakia katika klabu hiyo kutaonesha kushindwa kwa mchezaji huyo ambaye mwezi wa Julai alitoa taarifa akieleza kinagaubaga nia yake ya kuachana na City kwa sababu za kifamilia.

Wiki chache baadae, City ilikuwa imeingia matumaini kwamba makubaliano na klabu ya Corinthians kumuuza mshambuliaji huyo yatakamilika, lakini baadae klabu hiyo ya Sao Paulo-ilijitoa kwa sababu haikuweza kukamilisha taratibu za uhamisho kabla kufungwa kwa dirisha la usajili wao wa kimataifa.

Inter Milan pia imekuwa ikihusishwa na mchezaji huyo, lakini badala yake wakaamua kumchukua Diego Forlan kutoka Atletico Madrid kuchukua nafasi ya Samuel Eto’o. Mchanganyiko wa ada iliyokuwa ikitakiwa na Manchester City kwa ajili ya Tevez pamoja na mshahara wake ndio ilionekana kikwazo cha kumuuza mshambuliaji huyo.

Tevez bado hajapata nafasi ya kuanza mechi hata moja msimu huu kwa Manchester City, huku Sergio Aguero na Edin Dzeko wakionekana na Meneja Roberto Mancini wakakamavu katika safu ya ushambuliaji. Mshambuliaji pia alipoteza unahodha wake, nafasi iliyochukuliwa na Vincent Kompany na nafasi yake katika kikosi cha timu ya Argentina imechukuliwa na Aguero.

Tevez alisaini mkataba wa miaka mitano na City mwezi wa Julai mwaka 2009, akiwa ametokea klabu ya Manchester United. Aliwasilisha maombi ya uhamisho mwezi wa Desemba, kabla ya kuondoa maombi hayo na akaisaidia City kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya England.