Uadilifu unajenga imani za Wananchi-Dk Shein

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu-Zanzibar

UADILIFU unasaidia kujenga imani za wananchi kwa viongozi wao na watumishi wa umma na kuwafanya wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano wao wa dhati katika masuala mbali mbali ya maendeleo.

Hayo yameelezwa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein katika hotuba yake aliyoitoa katika Baraza la Idd El Fitri, huko Ukumbi wa Salama, katika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar, baada ya kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao umetoa mafunzo makubwa juu ya uadilifu.

Alisema kuwa uadilifu ni kipimo cha imani ya mtu na kumfanya awe raia mwema na kusisitiza kuwa mfanyakazi mwadilifu hutekeleza majukumu yake ipasavyo pamoja na kufika kazini kwa wakati na kuondoka kwa wakati. Alielendelea kueleza kuwa mfanyabiashara mwadilifu nae haghushi bidhaa na hakwepi kulipa kodi na mtumishi wa umma hatodai rushwa na mzazi mwadilifu hawezi kuitelekeza familia yake.

Rais Shein, alieleza kuwa mwezi wa Ramadhan uliomalizika haukuwa wa ibada tu bali ulikuwa wa mafunzo makubwa yakiwemo kula riziki za halali,kuepuka kusengenya, kutosema uwongo, kufanyiana ihsani, kuhurumiana, kusaidia, kufanya uadilifu na kuwa na tabia nzuri. Ni wajibu kuwafikiria wenye matatizo mbali mbali na kuwasaidia ambapo wenye uwezo wa mali wanawajibu wa kutoa zaka na sadaka, wazima wawasaidie wagonjwa na wenye mahitaji mbali mbali wakiwemo wasiojiweza na mayatima.

Dk Shein pia, alieleza umuhimu wa kuitumia vyema elimu za darsa zilizotolewa na Masheikh wakati wa mwezi wa Ramadhani kwa kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuleta matatizo yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya na maambukizo ya virusi vya Ukimwi mambo ambayo yanaathiri sana kundi la vijana.

Alisisitiza kuongezwa juhudi katika kuwahimiza watoto kutilia mkazo masomo yao na kutoa nasaha kwa wazazi kurudisha utamaduni wao wa zamamni wa kushirikiana katika malezi ya watoto.

Alisema kuwa Serikali kwa upande wake inajitahidi kuandaa mazingira mazuri yatakayowezesha watoto kupata elimu bora ambapo tayari ujenzi wa skuli mpya unaendelea na juhudi zinafanywa kuziimarisha zilizopo kwa kuzipatia samani, walimu, vitabu na vifaa vya maabara kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu nchini.

Alhaj Dk. Shein pia, alitoa shukurani zake kwa wakulima na wafanyabiashara kwa kusaidia katika upatikanaji wa chakula katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan pamoja na kutoa shukurani zake kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Maji (ZAWA) kwa juhudi zao za kuwapatia maji wananchi wanaoishai katika maeneo yenye upungufu wa maji.

Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeandaa mipango ya kuhakikisha inaongeza fursa zaidi za ajira rasmi na zile zisizo rasmi hapa nchini ambapo katika mwaka huu wa fedha serikali inatarajia kuajiri watu wapatao 2,476 kulingana na mahitaji na uwezo uliopo.

Dk. Shein alieleza kuwa serikali imeamua kuziimarisha shughuli za kilimo kwa kupunguza bei ya pembejeo za kilimo na huduma za matrekta ambapo tayari maandalizi yameanza kwa kuwaajiri mabibi na mabwana shamba wapya na kuimarisha.

Aidha, alitoa shukurani kwa wafanyakazi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuimarisha hali ya amani na utulivu hasa askari wa usalama barabarani kwa kusaidia kudhibiti ajali za barabarani katika mwezi wote Mtukufu wa Ramadhani.

Dk. Shein alitumia nafasi hiyo kwa kuwashukuru sana wakulima wa karafuu kwa namna wanavyounga mkono juhudi za Serikali za kuinua uchumi pamoja na wanavyounga mkono wito wa serikali wa kuziuza karafuu kwenye Shirika la Taifa la Biashara(ZSTC).

Alisema kuwa serikali imeshapanga mipango madhubuti ya kuliimarisha zao hilo na kuwalipa wakulima bei nzuri kulingana na bei ya soko la dunia na kuwanasihi wakulima kuendeleza ushirikiano na serikali katika kupambana na wafanya magenzo ya karafuu.

Viongozi mbali mbali wa serikali, dini na vyama vya siasa walihudhuria akiwemo Naibu Mufti Sheikh Saleh Omar Kabhi, Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Rais mstaafu Dk. Amani Abeid Karume, Mama Mwanamwema Shein pamoja na viongozi na wananchi mbali mbali.

Mapema Dk. Shein alihudhuria Sala ya Idd katika uwanja wa Maisara mjini Unguja na baadae alisalimiana na Masheikh na viongozi mbali mbali Ikulu mjini Zanzibar.