EU Kutenga Mabilioni Kukabiliana na Wahamiaji Kutoka Afrika

Baadhi ya wahamiaji kutoka Afrika.

Baadhi ya wahamiaji kutoka Afrika.


VIONGOZI wa Muungano wa Ulaya wanatarajiwa kutenga euro mabilioni ya fedha kwa mataifa ya Afrika kuyawezesha kusaidia kupunguza wimbi la wahamiaji Ulaya. Tume ya Muungano wa Ulaya ilisema itatoa kiasi cha euro bilioni 1.8 (£1.3bn) na huku ikiwa na imani kwamba mataifa zaidi ya Umoja wa Ulaya, EU yataahidi pesa zaidi ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Taarifa zaidi zinasema lengo la ufadhili huo ni kusaidia kusuluhisha matatizo ya kiuchumi na kiusalama ambayo huwafanya watu kutoroka mataifa ya Afrika. Aidha, zitatumiwa kuyashawishi mataifa ya Afrika kuwapokea watu ambao wamenyimwa hifadhi Ulaya. Ahadi hiyo inatarajiwa kutolewa kwenye mkutano mkuu utakaojadili kuhusu wahamiaji kutoka Afrika unaofanyika Malta, na ambao ulipangwa baada ya meli iliyobeba wahamiaji kuzama Libya mwezi Aprili na watu wanaokadiriwa 800 kufariki.

Watu 150,000 wamevuka Bahari ya Mediteranian kutoka Afrika mwaka huu huku idadi kubwa ikifikia nchini Italia na Malta. Hata hivyo, mtazamo wa EU umebadilika tangu Aprili na kuangazia zaidi wakimbizi wanaotoka mashariki na hasa Syria, ambao wanawasili kwanza Ugiriki na kuvuka hadi Uturuki kisha kuelekea kaskazini kupitia bataifa ya Balkan.

Zaidi ya viongozi 60 kutoka Afrika na Ulaya, akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, wanakutana Valletta, Malta kwa mkutano huo mkuu wa siku mbili kujadili uhamiaji. Tume ya Muungano wa Ulaya itaweka pesa hizo €1.8bn kwenye “hazina maalum” kwa ajili ya Afrika na imehimiza mataifa wanachama kufikisha kiasi hicho cha pesa. Hata hivyo, kuna shaka kuhusu iwapo mataifa hayo yatakubali wito huo.
-BBC