RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli, leo mchana amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukutana na hali ya kumsikitisha.
“Rais amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini. Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika Hospitali za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko”. Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema na kutoa maelekezo yafuatayo:
Rais amevunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ilishamaliza muda wake na amemteua Prof. Lawrence Mseru, kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili kuanzia kesho tarehe 10 Novemba, 2015.
Dk. Hussein L. Kidanto ambaye ndiye aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili sasa, amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine. Balozi Sefue pia amesema, Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo.
Tayari Wizara ya Fedha imetoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini. Hata hivyo Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote (Regular Maintenance).
Balozi Sefue pia metumia nafasi hii kuwaagiza watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.
“Hakutakuwa na huruma kwa watumishi wa Umma wasiojali wananchi na mahitaji yao” Amesisitiza Balozi Sefue.