Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Imesema katika majimbo manne kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa kwenye ujumlishaji matokeo, uliosababisha wabunge wa upinzani kutangazwa washindi.
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba jana aliwaambia wanahabari majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe. Alisema wanaamini wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana na utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye sheria.
Makamba alisema kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya.
“…Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa. Bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama kulikuwa na ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura. Hata hivyo,
tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya Ubunge, tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya wananchi, na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili tubaini makosa na kuyarekebisha,” alisema Makamba.
Akizungumzia waangalizi wa uchaguzi, alisema imefarijika kwamba karibu waangalizi wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi ulikuwa wa haki na huru, uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba changamoto zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa.
“…Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo sahihi cha utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka,” alisema.
Kwa upande wa Mgombea Urais tiketi ya CHADEMA, Edward Lowassa amegomea matokeo yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akidai matokeo hayo yamevurugwa kwa makusudi na watendaji ndani ya NEC kwa kusaidiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katikataarifa yake Lowassa kwa wanahabari alisema hatukubaliani na matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais, yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kote nchini na kuomba utangazaji usimamishwe na zoezi la kuhesabiwa lifanywe kikawaida na si kwa mifumo ya kompyuta.
“…Hii ni kwa sababu, upo ushahidi wa wazi unaothibitisha kwamba utangazaji wa matokeo hayo umevurugwa kwa makusudi na watendaji ndani ya NEC kwa kusaidiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Katika maeneo mengi ambako matokeo yameshatangazwa mpaka sasa, kilichoripotiwa kuwa matokeo ya uchaguzi wa urais, hakifanani wala kuendana na matakwa halisi ya wananchi. Matokeo mengi yamesheheni udanganyifu, ulaghai na yameandaliwa kwa lengo maalum la kumbeba mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli,” alisema Lowassa.
Aliongeza kuwa katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi, kura zetu zimepunguzwa na kuongezwa kwa mgombea wa CCM; maeneo mengine, kura zilizotangazwa zimetofautiana na idadi halisi ya kura zilizopigwa. “…Kwa mfano, matokeo yaliyotangazwa na NEC katika majimbo ya Mkoani na Mtambile, kisiwani Pemba, Makunduchi, Kiwengwa, Donge, Tunduru, Tunduma, Same Mashariki, Chambani, Tandahimba, Kilindi na kwingi kwingineko, ni miongoni mwa matokeo yanayothibitisha kuwa hiki kinachotangazwa na NEC, siyo kura za uchaguzi mkuu wa rais…,” alisisitiza Lowassa.
Aidha, aliongeza kuwa katika maeneo mengine, likiwamo jimbo la Ubungo, matokeo yaliyoko mikononi mwa msimamizi wa uchaguzi, yanatofautiana na yale ambayo yamekusanywa kutoka katika vituo vyote vya jimbo hilo. “…Hali kama hiyo ipo pia katika majimbo yote ambayo wagombea wa CHADEMA na wale wa vyama washirika vya CUF na NCCR – Mageuzi, ama wamekuwa na nguvu kubwa au wameibuka washindi. Upo ushahidi wa wazi ambao, ninyi waandishi mnaweza kwa kutumia uandishi wenu kuuthibitisha kwamba, katika majimbo yote ambako wagombea wa UKAWA wameshinda, TUME imechelea kutangaza matokeo ya urais kwa sababu zinazothibitisha kuwapo kwa mikakati ya hila.”
Alisema kwamba matukio yote ya NEC kutangaza matokeo yaliyochakachuliwa yamekuja baada tu ya Jeshi la Polisi kuvamia vituo vyetu vitatu vya kuhesabia kura na kuwakamata wataalam wetu waliokuwa wakipokea matokeo ya kura za rais nchi nzima ambayo hadi uvamizi huo ulipofanyika tulikuwa tukiongoza katika maeneo mbalimbali.
“…Tunaamini kwa dhati kwamba, uvamizi huo ulifanyika mahususi kwa malengo ya kufanikisha uchakachuaji huo ambao sasa tunauona ukiendelea kufanyika kupitia matangazo yanayoendelea kutolewa sasa na NEC. Wakati tukijua kwamba NEC ndiyo mamlaka pekee ya kisheria ya kutangaza matokeo ya urais, tunapenda kuwa taarifu Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwamba hadi wakati uvamizi huo ulipofanyika kura zetu za urais tulizokuwa tumezikusanya zilikuwa zikionyesha tukiongoza kwa asilimia zaidi ya 60.”
“Kutokana na makosa hayo makubwa na ya makusudi yanayofanywa na watendaji wa NEC, mimi Edward Ngoyai Lowassa, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano na Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji, tunautangazia umma wa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa, kwamba hatukubaliani na matokeo yanayotangazwa na NEC.” Alisema.