Tume ya Uchaguzi Zanzibar Yafuta Uchaguzi Mkuu, NEC Yajiengua…!

Mwenyekiti ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Mwenyekiti ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Na Mwandishi Wetu
*Lowassa Agomea Matokeo ya Urais NEC…
TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imefuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mjini humo kutokana na dosari kadhaa zilizojitokeza wakati wa zoezi zima. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salim Jecha kwa vyombo vya habari alisema dosari zilizojitokeza ndizo zilizochangia kucheleweshwa kwa matokeo hayo.

Mwenyekiti huyo alizitaja miongoni mwa dosari zilizojitokeza kuchangia kufutwa kwa uchaguzi huo ni pamoja na kutofahamiana kwa wajumbe wa ZEC kiasi cha kupigana, baadhi ya makamishna wa ZEC kuonekana kuwa wawakilishi wa vyama vyao, uwepo wa dosari nyingi ikiwa ni pamoja na vituo vya kupigia kura kuwa na idadi kubwa ya kura zaidi ya wapigakura wa kituo hasa Pemba.

Alisema sababu nyingine ni pamoja na kitendo cha wasimamizi wa uchaguzi kuhamisha masanduku ya kura na kuhesabia nje ya vituo husika, kutolewa nje kwa baadhi ya mawakala wakati wa zoezi la kuhesabu kura Pemba, kuvamiwa kwa baadhi ya vituo na makundi ya vijana na kupigwa na kuzuia baadhi ya watu kupiga kura.

Sababu nyingine alisema ni pamoja na baadhi ya vyama kuingilia majukumu ya ZEC kwa kujitangazia ushindi kabla ya kutangazwa, kuwepo na malalamiko mengi kutoka katika vyama vilivyoshiriki uchaguzi na uwepo wa dosari katika fomu za matokeo hasa kutoka pemba jambo ambalo limezua ulakini.

“…Kwa kuzingatia hayo na mengine ambayo sijayaeleza, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi hivyo kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi,” alisema Jecha katika taarifa yake.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva.

Hata hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) imesema haiwezi kuathiriwa na kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kwa kuwa hadi uchaguzi huo unafutwa wao tayari walikuwa wamepokea matokeo ya kura za urais kutoka Zanzibar na kuyaingiza katika mfumo wa matokeo hivyo wataendelea kutangaza matokeo yao kama kawaida.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva akizungumza na vyombo vya habari alisitiza uchaguzi uliofutwa ni wa Zanzibar na si wa Tanzania Bara hivyo hawaathiriki na matokeo ya kufutwa kwa uchaguzi huo kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu na wachambuzi wa kisiasa. Aliwataka Watanzania kuendelea kufuatilia matokeo yao kama kawaida.

Wakati huo huo; tayari Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa pamoja na mgombea mwenza kutoka Zanzibar, Duni Haji ametangaza kutoyatambua matokeo ya urais yanayoendelea kusomwa na NEC wakidai yanatolewa baada ya kuchezewa (kuchakachuliwa) na kuiomba tume kusitisha na kuanza kuyahakiki upya na pia kuyajumlisha kwa mfumo wa kawaida na sio kama ilivyo sasa.

Lowassa alisema matokeo hayo yanatofautiana na nakala za matokeo za mawakala wao vituoni na zoezi la uchakachuaji lilianza baada ya Jeshi la Polisi kuvamia na kuwakamata vijana wa chama cha Chadema ambao walikuwa wakifanya kazi ya kujumlisha matokeo wanayoyapokea kutoka kwa mawakala wao vituoni nchi nzima.

Kwa upande wa Zanzibar mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha CUF, Seif Sharif Hamad ameupinga uamuzi wa ZEC kuufuta uchaguzi wa Zanzibar akidai ni maamuzi ya Mwenyekiti wa ZEC binafsi bila kuwashirikisha makamishna wenzake jambo ambalo ni kinyume na sheria. Seif ametoa tamko la kupinga na kulaani tukio hilo huku akiviomba vyombo vya kimataifa na Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati ili kunusuru mgogoro huo.

Hata hivyo amewataka wananchi na wanaCUF kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati ambapo viongozi wao wanapambana kuhakikisha haki na maamuzi yao ya kura yanalindwa na kuheshimiwa. Amewahakikishia watapambana kuhakikisha haki inapatikana kwa mujibu wa sheria na taratibu.