MATOKEO ya Uchaguzi Mkuu nafasi za madiwani, wabunge na urais uliofanyika jana maeneo mbalimbali nchini Tanzania yameanza kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huku vyama vya CHADEMA na CCM vikionekana kuchuana vikali na kufuatiwa na Chama cha Wananchi, CUF hasa Zanzibar.
Kwa mujibu wa matokeo ambayo yametangazwa CCM imeshinda katika Majimbo ya Makunduchi, Mtambile, Kibaha Mjini, Ndanda, Nsimbo, Bumbuli, Donge, Paje, Lulindi, Kongwa, Mpwapwa, Chemba, Mbinga Mjini, Nanyamba, Mkinga, Pangani, Lushoto na Jimbo la Peramiho. Majimbo mengine yaliotwaliwa na CCM hadi sasa ni pamoja na Njombe Mjini, Singida Mjini, Geita Vijijini, Ilemela Bukoba, Njombe Mjini, Ilala na Jimbo la Lindi Mjini.
Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) majimbo waliotangazwa kutwaa ni pamoja na Jimbo la Hai, Jimbo la Mkoani, Kiwani, Chambani, Mbeya Mjini, Tanga Mjini, Moshi Mjini, Jimbo la Bunda na Jimbo la Arumeru Mashariki. Hata hivyo pamoja na hivyo ukijumlisha majimbo ambayo mpaka sasa CCM imeshinda yanafikia Majimbo 26 na CHADEMA majimbo 12 na CUF 14 huku chama kimpya cha ACT kikiwa na Jimbo moja hadi sasa.
Mwandishi wa habari hizi alitembelea pia katika kituo cha majumuisho ya kura cha Jimbo la Segerea ambapo bado kura zinahesabiwa lakini matokeo ya awali kwa Kata za Jimbo hilo yakiwa yametoka ambapo; Kata ya Tabata mshindi aliyetangazwa ni Chadema (9,956), Kata ya Segerea mshindi pia ni Chadema (8,295), Kata ya Buguruni mshindi ni CUF (11,881), Kata ya Kinyerezi mshindi ni Chadema (8,900). Huku kwa Kata ya Ubungo ambapo ni Jimbo la Ubungo mshindi ni Chadema (14,344).
Maeneo mengine bado kura zinaendelea kuhesabiwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu, Damian Lubuva (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari na waangalizi wa kimataifa wakati akitangaza matokeo ya awali ya urais Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima.