Na Mwandishi wetu
TIMU ya Taifa ya Algeria (Desert Warriors) itawasili Septemba Mosi mwaka huu saa 2.50 usiku kwa ndege maalum.
Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari.
Wambura amesema Algeria inawasili kucheza mechi ya mchujo kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Equatorial Guinea na Gabon.
Akifafanua zaidi amesema, mechi hiyo itachezwa Septemba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Viingilio kwa mechi hiyo ni viti vya kijani ni sh. 3,000, viti vya bluu sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, VIP C sh.10,000, VIP B sh. 20,000 na VIP A sh. 30,000. Tiketi zitaanza kuuzwa Septemba Mosi mwaka huu.
Amesema vituo vya kuuza tiketi ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha Mafuta cha Big Bon (Kariakoo), Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora na Ohio, Uwanja wa Uhuru na Kituo cha Mafuta cha OilCom Ubungo.
Wambura amesema tayari mchezaji Idrisa Rajab anayechezea Sofapaka ya Kenya amewasili jana usiku na tayari ameripoti kwenye kambi ya Taifa Stars. Stars inaendelea na mazoezi Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
Aidha akizungumzia mashtaka ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu kwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wake Alfred Tibaigana iliyokuwa ikutane jana.
Amesema kamati imeahirisha kikao chake cha kusikiliza malalamiko dhidi ya Rage na Sendeu. Kwa mujibu wa Tibaigana, kikao kimeahirishwa kutokana na Kamati kutotimiza akidi (column) kwa wajumbe wake. Walalamikiwa wataarifiwa siku ambayo kikao kitapangwa tena.
Wakati huo huo, Wambura amesema aliyekuwa kipa wa Yanga, Ivan Knezevic ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na Chama cha Mpira wa Miguu cha Serbia (FAS) ili kujiunga na klabu yake mpya nchini humo.
Knezevic ameombewa ITC kama mchezaji wa ridhaa katika klabu ya FK Borac ya nchini humo. TFF itampatia hati hiyo kwa vile mkataba wake katika klabu ya Yanga ulikuwa umemalizika.
Aliongeza kuwa, Kamati ya Waamuzi ya TFF imeteua watathmini 11 wa waamuzi (referees assessors) kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom. Watathmini hao watasimamia baadhi ya mechi za ligi hiyo.
Walioteuliwa ni Alfred Lwiza (Mwanza), Soud Abdi (Arusha), Charles Mchau (Kilimanjaro), Manyama Bwire (Dar es Salaam), Joseph Mapunda (Ruvuma), Isabela Kapela (Dar es Salaam), Paschal Chiganga (Mara), Emmanuel Chaula (Rukwa), Mchungaji Army Sentimea (Dar es Salaam), David Nyandwi (Rukwa) na Leslie Liunda (Dar es Salaam).