Akizungumza na wandishi wa habari badaa ya kukutana na Mkurugenzi wa Kampuni ya China Merchants Group itakayosimamia ujenzi huo, Dk Hu Jianhao, Membe alisema katika ujenzi huo utakaochukua hekta 2400, wananchi wote watakaohuswa hawataachwa bure.
“Mradi huo ni mkubwa sana unaoshirikisha kampuni hii ya China Merchants Group, wawekezaji kutoka Oman ambao wataalamu wao pia wameshafika na Serikali ya Tanzania. Tunatarajia kuwa utaibadilisha Bagamoyo kwa kiasi kikubwa na kuufannya kuwa mji wa viwanda, hatua itakayovuta wawekezaji wengi zaidi na kuzalisha ajira nyingi,” alisema.
Mradi mzima wa ujenzi utajumuisha eneo hekta 800 kwa ajili ya ujenzi wa bandari na eneo la hekta 1,700 kwa ajili ya ukanda wa viwanda. Mazungumzo hayo ni sehemu ya awali ya maandalizi kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari hiyo, katika sherehe inayotarajiwa kuongozwana Rais Jakaya Kikwete leo.
Mradi huo wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo utakaokuwa wa aina yake Afrika Mashariki na Kati, unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 10 na kukamilika kati ya miaka mitano hadi saba ijayo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Dk Florens Turuka jana, Rais Kikwete ataweka jiwe hilo la msingi kwa ajili ya uzinduzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo.
Eneo hilo litaendelezwa chini ya makubaliano ya Serikali ya Tanzania, Kampuni ya China ya Merchants Holdings International (CMHI) na Mfuko wa Taifa wa Dharura wa Oman (SGRF). Chini ya ushirikiano huo, Serikali inawakilishwa na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Oman itawakilishwa na SGRF na China CMHI.
Dk Turuka alisema mradi huo pia utahusisha ujenzi wa miundombinu kama vile reli, mitandao ya barabara, umeme, umeme, gesi na mitandao ya mawasiliano. Mradi huo unatarajiwa kuibadili Tanzania na kuwa kituo kikuu cha usafirishaji kwa wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa ambao wataunganishwa na viwanda vitakavyozalisha bidhaa zilizoongezewa ubora.
Kwa mujibu wa Dk. Turuka, wazo la kuwepo mradi huo, limetokana na uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia baina ya Tanzania, China na Oman katika kuhamasisha uimarishaji wa viwanda Afrika jambo litakalosaidia kuongeza ajira nchini. Kuanzishwa kwa mradi huo, kuliibuka tangu mwaka 2008, Rais Kikwete alipotembelea China na kuzungumza na Rais wa nchi hiyo, Hu Jintao, na kuafikiana kujenga bandari hiyo.
Sherehe za kuweka jiwe la msingi zitahudhuriwa na wageni wa kimataifa na wa ndani wakiwemo wawekezaji katika mradi huo. Wengine wanoatarajiwa kuhudhuria ni wanadiplomasia na ujumbe kutoka kwa Sultani wa Oman utakaoongozwa na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano nchini humo, Shehe Abdullah Al Saadi.