Jotoardhi Kuinufaisha Kisaki

Kisaki Hot Spring Tembea Tanzania
Na Lilian Lundo – Maelezo
Wananchi kata ya Kisaki, wilaya ya Morogoro Vijijini kunufaika na nishati ya jotoardhi inayotokana na chanzo cha maji ya moto yaliyoko katika kata hiyo.
Akiongea na kamati ya maendeleo ya kata ya Kisaki leo, Mkurugenzi Mhandisi Kato Kabaka wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania aliiambia kamati hiyo kuwa, Kisaki ni mojawapo ya Kata ambazo zitanufaika na nishati ya umeme itokanayo na jotoardhi.
“Jotoardhi ni nishati ya gharama nafuu ambayo ni jadidifu, yaweza kuvunwa kwa miaka mingi bila kuisha tofauti na nishati zingine zinazo athiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi, hivyo mitambo yake itakapowashwa haitazima labda pale tu patapohitajika marekebisho ya kiufundi.” Alisema Bwana Kato.
Bwana Kato aliongezea kwa kusema kuwa, Jotoardhi ina faida mbadala mbali na nishati ya umeme. Faida hizo zinatokana na joto na kemikali ambazo zinapatikana katika majimoto ambayo hutumika kukausha mazao, kuogeshea mifugo, kutumika katika kilimo, ufugaji wa samaki pamoja na kutumika katika mabwawa ya kuogolea kwenye mahoteli ya kitalii na hata majumbani.
Kupitia kikao hiko Bwana Kato aliiomba kamati hiyo kuukubali mradi huo ili Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania iweze kuendelea na utafiti wa jotoardhi katika kata ya Kisaki hatimaye wananchi waweze kunufaika na nishati hiyo pindi mradi huo utakapokamilika.
Kamati imeupokea mradi huo, na kusema umekuja wakati muafaka kwani kata ya Kisaki haijafikiwa na umeme. Hivyo mradi huo utawanufaisha kwa kuwaletea umeme katika vijiji vyao.
Jotoardhi ni mojawapo ya chanzo cha nishati kinachotumia joto lililopo katika gamba la dunia. Joto hili linatokana na mchakato wa ndani ya tufe la dunia na kiasi kidogo jotojua linapokelewa kwenye uso wa dunia.
Maeneo mengine yenye viashiria vya jotoardhi ni Ziwa Manyara, Kreta ya Ngorongoro, Utete (Pwani), Luhoi (Pwani) Songwe (Mbeya), Ngozi, Rukwa, Kilambo, Mampulo, Ibadakuli(Shinyanga), Mtagata (Kagera), Dodoma, Singida na Tanga.
Serikali ilianzisha kampuni hii ya kuendeleza nishati ya jotoardhi (Tanzania Geothermal Development Company Limited -TGDC) mwaka 2013 ili kufanya tafiti za kina na kuendeleza kwa haraka nishati ya jotoardhi nchini ili kufikia mwaka 2020 taifa liwe na megawati 200 zinazozalishwa kwa jotoardhi.