Rais Azindua Bomba la Gesi Madimba

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na  Alhaj Aliko Dangote na ujumbe wake kutoka Nigeria wakipata picha ya kumbukumbu wakati wa sherehe za kuzindua kiwanda hicho kikubwa kuliko viwanda vyote vya saruji Afrika Mashariki huko Mtwara Jumamosi Oktoba 10, 2015

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Alhaj Aliko Dangote na ujumbe wake kutoka Nigeria wakipata picha ya kumbukumbu wakati wa sherehe za kuzindua kiwanda hicho kikubwa kuliko viwanda vyote vya saruji Afrika Mashariki huko Mtwara Jumamosi Oktoba 10, 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete , Jumamosi, Oktoba 10, 2015 amezindua mtambo mkubwa na miundombinu ya kisasa kabisa ya kuchakata na kusafirisha gesiasilia katika uwekezaji mkubwa ambako Serikali imewekeza kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.33, sawa na sh trilioni 2.926, na kukamilisha uhakika wa kuongeza upatikanaji wa gesi kwa ajili ya matumizi ya uzalishaji na matumizi ya umeme viwandani, majumbani na kwenye magari.
Rais Kikwete amezindua mtambo huo katika eneo la Madimba, kilomita 25 kutoka mjini Mtwara, na kwa kuzindua miundombinu hiyo, Serikali sasa imekamilisha uunganishaji wa maeneo yanayozalisha gesiasilia kwa sasa ya Mnazi Bay na Songo Songo yanayotarajiwa kuzalisha gesi baadaye ya Ntorya, Kiliwani Kaskazini (Songo Songo) katika Mkoa wa Mtwara na Mkuranga katika Mkoa wa Pwani pamoja na gesi itakayotoka Bahari ya Hindi.
Akizungumza katika sherehe kubwa ya uzinduzi iliyohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi, mabalozi, wawekezaji katika sekta ya gesiasilia nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dr. James Mataragio amemwambia Rais Kikwete kuwa fedha za kuwekeza katika mradi huo mkubwa zimetokana na mchango wa Serikali ya Tanzania na mkopo kutoka Serikali ya Watu wa China kupitia benki yao ya EXIM.
Miundombinu hiyo iliyozinduliwa na Rais Kikwete inahusisha mitambo ya Madimba yenye uwezo wa kusafisha gesi futi za ujazo milioni 210 kwa siku, mitambo mingine kama hiyo katika eneo la Songo Songo yenye uwezo wa kusafisha gesi futi za ujazo zipatazo milioni 140 kwa siku, bomba lenye urefu wa kilomita 18 kutoka eneo la Mnazi Bay, Msimbati hadi Madimba na bomba la kusafirisha gesiasilia kutoka Mabimba hadi Kinyerezi mjini Dar es Salaam lenye urefu wa kilomita 477.
Aidha, mitambo hiyo ni pamoja na bomba la kusafirishia gesi la kilomita 29 kutoka Bahari ya Hindi hadi Songo Songo hadi Somanga Fungu na bomba lenye urefu wa kilomita 28 kutoka Kinyerezi hadi Ubungo hadi Tegeta kwa ajili ya kuzalisha umeme zaidi nchini.
Ujenzi wa miundombinu hiyo ulianzishwa na Rais Kikwete wakati shughuli rasmi ya utandazaji bomba kutoka Madimba hadi Dar es Salaam Novemba 21 mwaka 2012 wakati alipoweka jiwe la msingi katika ujenzi wake eneo la Kineyerezi Dar es Salaam na hivyo kuwezesha wakandarasi wakuu kuanza kazi ya ujenzi wa miundombinu hiyo ambayo inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania kupitia TPDC.
Wakandarasi wakuu watatu ni makampuni matatu kutoka China ambayo ni Kampuni ya China Petroleum Technology and Development Corporation (CPTDC), China Petroleum Pipeline Bureau (CPP) na China Petroleum Engineering Company (CPE). Makampuni hayo yote matatu ni tanzu ya Shirika la Mafuta la China la China National Petroleum Company (CNPC).
Mkurugenzi huyo wa TPDC ambayo inashiriki katika Mradi wa miundombinu hiyo kupitia kampuni yake tanzu ya GASCO amesema kuwa uzinduzi wa miundombinu unaifanya Tanzania kuingia katika orodha ya nchi zenye nishati ya gesiasilia duniani. “Na siyo ya kutosha tu bali ya kukidhi mahitaji muhimu kwa uwekezaji mkubwa, wa kati na hata wa kijasiriamali na hivyo kuwa na msingi mkuu na muhimu wa kuchochea maendeleo ya viwanda na ukuaji wa uchumi wa kasi zaidi.”
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Kikwete ametaka wote wanaohusika na huduma ya umeme kuhakikisha wanakomesha kukatika kwa umeme nchini kwa sababu sasa hakuna sababu ya kuwepo kwa tatizo hilo nchini.
Aidha, ameitaka TPDC kutimiza wajibu wake wa kijamii kwa kuwajengea wananchi huduma za afya, zahanati, shule na mahitaji mengine madogo wakazi wa maeneo ambako gesi hiyo inatoka na hata katika maeneo ambako bomba lao kuu linapitia.