Kanali Gaddafi ‘bado tishio’ Libya

Waasi nchini Libya

MKUU wa waasi nchini Libya amesema, Kanali Muammar Gaddafi bado ni tishio nchini humo na duniani kwa ujumla. Mkuu wa Baraza la mpito la taifa (NTC), Mustafa Abdul Jalil amesema majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya, Nato, na washirika wengine lazima waendelee kuwaunga mkono waasi dhidi ya ‘mtawala wa mabavu.’

Waasi wameudhibiti mji mdogo wa Nofilia wakielekea kwenye ngome ya Kanali Gaddafi- na mji alipozaliwa-Sirte. Hadi sasa haijulikani Kanali Gaddafi alipo tangu waasi walipoingia Tripoli wiki iliyopita, na kuteka makazi yake. Tayari wanadhibiti eneo kubya ya Libya, baada ya mapigano yaliyodumu kwa miezi kadhaa tangu maandamano yalipoanza.

Akizungumza katika mkutano wa wakuu wa majeshi ya ulinzi huko Qatar, mkuu wa NTC, Mustafa Abdul Jalil, alisema majeshi ya Kanali Gaddafi bado yanaweza kujibu mashambulizi hata baada ya waasi kupambana dakika za mwisho na majeshi yanayomwuunga mkono Gaddafi.

Waasi wanasema wako katika mazungumzo na viongozi wa kikabila wa Sirte ili kuzuia umwagikaji damu, lakini mpaka sasa hawajafanikiwa. Mwandishi wa BBC Paul Wood ambaye yupo na waasi wakielekea Sirte alisema, huenda ikawa bado viongozi wa kikabila wanayo akilini onyo alilotangaza Kanali Gaddafi kuwa waasi wanaingia mjini humo kupora na kubaka wanawake.

Huku majeshi ya kivita yakiendelea kuwaunga mkono waasi, waasi wanatarajiwa kupigana kwa kile kinachoonekana kuwa makali ya mwisho ya vita hivi na kwa ajili ya mapinduzi yao. Azimio la Nato linaendelea mpaka mwisho wa Septemba ambapo itabidi ipitiwe upya na nchi wanachama wote.
-BBC