Uhuru Ateta na JK

Rais Uhuru-Kenyatta-
Serikali ya Kenya na watu wake wameelezea shukrani zake kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa urafiki na ushirikiano thabiti aliouonyesha kwa watu wa Kenya katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema hayo tarehe 5 Oktoba, 2015 katika Ikulu ya Nairobi wakati wa mazungumzo ya kiserikali.

“I thank you, and on behalf of People of Kenya for your friendship and Cooperation that was reflected during your 10 years as President” Rais Kenyatta amemueleza Rais Kikwete wakati wa mazungumzo yao jijini Nairobi.

“Chini ya uongozi wako Kenya na Tanzania zimeongeza ushirikiano baina yao katika miundombinu, biashara, uwekezaji, sekta binafsi na biashara ambapo imeongezeka na kuifanya Tanzania kuwa soko kubwa la Kenya” Rais Uhuru amesema.

Rais Kikwete yuko nchini Kenya kwa Ziara ya kiserikali ya siku tatu, ambapo pamoja na mambo mengine , Rais Kikwete atahutubia Bunge la Kenya na kukutana na wafanyabiashara wa nchini Kenya.

Mara baada ya kuwasili jumapili jioni Rais Kikwete alikutana na Watanzania waishio nchini Kenya na kula nao chakula cha usiku katika Hoteli ya Villa Rosa Kempisky. Watanzania hao wamemshukuru Rais na kumpongeza kwa mafanikio yanayoshuhudiwa nchini.

Akisoma risala yao Makamu mwenyekiti wa umoja wa Watanzania waishio nchini Kenya, Bw Cleophas Tesha amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi binafsi za Rais Kikwete na Serikali ambayo ameisimamia kwa miaka yote 10.

“Kwa Umakini wako katika kusimamia maslahi ya wananchi, uimara wako bila kushinikizwa, tunakupongeza kwa kuweka nchi yetu katika ramani ya dunia”. Amesema Bw. Tesha “Tunaamini bado Taifa litaendelea kutumia ujuzi wako”. Leo Usiku Rais Kikwete na ujumbe wake watahudhuria dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake.

Kesho tarehe 6 Rais Kikwete anatarajia kuhutubia Bunge la Kenya na wananchi wake ambapo anatarajia kuwaaga rasmi Rais Kikwete na ujumbe wake wanatarajia kuondoka Nairobi kurudi Dar-es-Salaam.