Rais Kikwete aanza ziara rasmi ya Kenya

Jakaya-Kikwete
• Aungana na Rais Kenya kufungua barabara itayounganisha Tanzania na Kenya.

• Kuhutubia Bunge na kutembelea Kaburi la Hayati Jomo Kenyatta

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Jumapili, Oktoba 4, 2015 ameanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu katika Jamhuri ya Kenya kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta ambako miongoni mwa shughuli nyingine atahutubia Bunge la Kenya.

Rais Kikwete ameanza ziara yake kwa kuungana na Rais Kenyatta kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Taveta-Mwatate ambayo ni sehemu ya barabara inayounganisha Tanzania na Kenya ikianzia Arusha-Holili-Taveta-Mwatate. Barabara hii itaunganisha eneo la kaskazini mwa Tanzania na Bandari ya Mombasa, Kenya.

Hii ni ziara ya pili rasmi kwa Rais Kikwete katika Kenya. Miaka mitatu iliyopita, Rais kikwete alifanya ziara rasmi katika Kenya kwa mwaliko wa Rais Mwai Emilio Kibaki na Rais Kikwete ataitumia ziara ya sasa kuwaaga wananchi wa Kenya baada ya miaka 10 ya uongozi ambako ameimarisha sana uhusiano kati ya Tanzania na Kenya ikiwa ni pamoja na kusaidia kusuluhisha mgogoro mkubwa wa kisiasa uliosababisha machafuko na mauaji ya mamia ya wananchi wa Kenya kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2009.

Mbali na kuwaaga wananchi wa Kenya katika nafasi yake kama Rais wa Tanzania, Rais Kikwete pia atawaaga viongozi na wananchi wa Kenya kwenye nafasi yake kama Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).

Aidha, mbali na kuhutubia Bunge la Kenya wakati wa ziara yake, Rais Kikwete atatembelea na kuweka shada la maua kwenye kaburi ya Hayati Jomo Kenyatta, Rais wa kwanza na muasisi wa Taifa la Kenya.

Rais Kikwete pia atafanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali na mwenyeji wake, Rais Kenyatta; atahutubia Chama cha Wafanyabiashara wa Kenya na atatembelea Kiwanda cha Dawa cha Universal kilichoko eneo la Kikuyu.

Katika tukio lake la kwanza, Rais Kikwete na mwenyeji wake kwa pamoja wameanzisha rasmi ujenzi wa Barabara ya Arusha-Holili-Taveta-Mwatate kwa kiwango cha lami kwa kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa kipande cha Taveta-Mwatate chenye urefu wa kilomita 98.4 na kilomita nyingine tisa za lami ambazo zitajengwa katika mji wa Taveta.

Barabara ya Taveta-Mwatate ambayo ujenzi wake utachukua miezi 36 ilianza kujengwa Mei 17, mwaka jana, 2014, inatarajiwa kukamilika Mei 17, mwaka 2017, kwa gharama ya shilingi za Kenya bilioni 8.4 ambazo zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Kenya. Tayari kilomita 34 za barabara hiyo zimejengwa kwa lami.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Mwakilishi wa AfDB, Bwana Gabriel Negatu amesema kuwa barabara hiyo ni sehemu ya mtandao wa barabara za kuunganisha nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC). Moja ya barabara hizo ya Arusha-Namanga-Athi River tayari imekamilika na kufunguliwa rasmi na viongozi wa EAC.

Bwana Negatu amesema kuwa AfDB imezitengea Tanzania na Kenya dola za Marekani bilioni 1.5 kwa ajili ya miradi ya miundombinu na kuwa kati ya hizo tayari dola milioni 218 zimetolewa milioni 112 zikiwa zimetolewa kwa Tanzania na milioni 106 zimetolewa kwa Kenya.